The House of Favourite Newspapers

Matajiri wa Zambia watua kuwafuata Msuva, Ngoma Dar

Ibrahim Mussa | ChampioniDar es Salaam

 

UONGOZI wa Klabu ya Zanaco ya Zambia umepanga kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa ili kufanya mazungumzo na wachezaji wawili wa Yanga, Simon Msuva na Mzimbabwe, Donald Ngoma baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kuvutiwa na uwezo wao.

Zanaco inayomilikiwa na Benki Kuu ya Biashara nchini Zambia ambayo inatajwa kuwa kati ya timu tajiri kwa ukanda huu, imeonyesha nia ya wazi ya kutaka kuwachukua wachezaji hao baada ya kuwaona katika michezo waliyocheza na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kupata nafasi ya kusonga mbele hatua ya makundi kwa faida ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya sare ya 1-1, ugenini na suluhu nyumbani.

Awali kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia, Numba Mumamba, alithibitisha kumhitaji Msuva ndani ya kikosi chake iwapo watafanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo ambapo ilikuwa kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Yanga ambao umewapa nafasi ya kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.

Donald Ngoma (kulia).

Akizungumza na Championi Jumatano moja kwa moja kutoka Lusaka, Zambia, Mumamba alisema kuwa itakuwa vizuri kama uongozi wa timu yake utakamilisha taratibu za kuwanasa wachezaji hao kwa hatua inayofuata katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana kuridhishwa na viwango vyao.

“Nimeshazungumza na uongozi juu ya wachezaji hao na kama yule anayevaa jezi namba 27 (Msuva) ni mchezaji hatari kutokana na kutumia akili nyingi uwanjani, uongozi bado unaendelea kufuatilia taarifa zake muhimu hasa kuhusu ukubwa wa mkataba wake, maana wakati wowote wanaweza kufika huko kuona jinsi gani wanazungumza na Yanga ili aongeze nguvu katika timu yetu.

“Lakini sijamuona huyo peke yake, yupo na mwingine aliyecheza namba tisa katika mchezo wa kwanza ambapo alivaa jezi namba 11 (Ngoma), huyu hakuwepo katika mchezo wa marudiano hapa Zambia, lakini naye yupo katika mipango yangu kama atakuwa tayari kujiunga na sisi katika hatua inayofuata tutamchukua.

“Tunajua uwezo wa kufanya hivyo tunao ila sijajua wachezaji wenyewe kama wao wapo tayari kujiunga na kikosi chetu,” alisema Mumamba.

Ikumbukwe kuwa Msuva amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ndani Yanga wakati Ngoma mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Comments are closed.