The House of Favourite Newspapers

NUH: Nilikula Mikwara Nikabadili Dini

STORI: NA PHILLIP NKINI |CHAMPIONI JUMATANO| Dar es Salaam

MUZIKI wa Bongo Fleva, umekuwa ukipanda kwa kasi ya hali ya juu sana kwa siku za hivi karibuni. Kila msanii amekuwa akifanya ubunifu wake ili kuhakikisha anakwenda juu na kujikusanyia mashabiki wengi kadiri siku zinavyozidi kusonga. Umaarufu wa msanii yeyote yule unakuja kutokana na kazi bora ambazo amekuwa akifanya kwa ubunifu wa hali ya juu.

 

Pamoja na Tanzania kuwa na wasanii wengi, lakini kuna msanii anaitwa Nuh Mziwanda ambaye nyimbo zake za hivi karibuni zimekuwa zikiteka masikio ya watu wengi kwa kasi ya hali ya juu.

Pamoja na kutanua na wimbo wa Jike Shupa, ambao ulifanya vizuri sana mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, sasa Nuh amerejea na wimbo mwingine unaoitwa Anameremeta.

Huu ni wimbo ambao watu wengi wamekuwa wakiufurahia kwa jinsi midundo yake ilivyo na aina ya ubunifu uliotumika.

Championi limefanya mahojiano na Nuh, ambapo msanii huyo amefunguka mambo mengi ikiwemo uhusiano wake na Ali Kiba, mke wake, maisha ya ndoa na mwenendo mzima wa muziki wa kisasa.

“Watu wengi wamekuwa wakishindwa kunielewa vyema, lakini mimi sikuanza kama mwanamuziki, nilikuwa prodyuza wa nyimbo za Kwaya.

“Huko ndiko nilipoanzia na kupatia umaarufu, wanakwaya, vikundi na hata viongozi wa makanisa wengi wakanifahamu kutokana na kazi hii.

“Nimelelewa kwenye dini kali sana ya Kikristo, baba yangu alikuwa anapiga kinanda kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Kariakoo, mama yangu ni mwimba kwaya kwenye kanisa hilohilo, hapa utaona ni jinsi gani kwetu dini imetawala.

“Nimefanya kazi huko kwa muda mrefu sana, baadaye nikahamia Sinza, nakumbuka ofisi ilikuwa Sinza Palestina, lakini baadaye nikawaomba wazazi wangu niingie kwenye kuimba mwenyewe.

“Walijua labda nataka kuimba gospo, lakini nilipowaeleza ni Bongo Fleva waligoma, nikawaomba sana baadaye wakakubali, wimbo wangu wa kwanza ulikuwa wa rapu ambao uliitwa Bwege Mtozeni, huu haukufanya vizuri hata kidogo.

Nikaachana na kurapu na kutoa wimbo mwingine uliojulikana kwa jina la Filling Love, nao haukufanya vizuri pia,” anasema Nuh huku akicheka.

Mwanamuziki huyo ambaye anaishi kwenye jumba la ghorofa eneo la Ubungo External, anasema baada ya hapo alimtafuta rafi ki yake wa muda mrefu, Ali Kiba na kufanya naye kolabo ya wimbo wake unaoitwa Mniache.

“Unajua watu wengi wanafi kiri kuwa mimi na Ali tumejuana kwenye Jike Shupa, hapana hata kidogo, mimi nimekuwa na Ali kama mtu na kaka yake, nilianza kuimba naye tukiwa chini sana na nimekuwa nikimheshimu naye ananisheshimu.

“Wimbo wangu wa tatu unaoitwa Mniache, niliimba naye na hata leo nikitaka kuimba na Ali wala situmii nguvu kubwa, namwambia tu naomba nikushirikishe kwenye wimbo wangu, najua hawezi kukataa, hapo biashara inaisha.

“Nikipata shida hapa nampigia Ali namwambia nimepata shida f’lani na baada ya dakika tano unamuona mlangoni, huyu mimi ni kaka yangu siyo kwamba tumejua leo wala jana.

“Hata wimbo wa Jike Shupa, yeye ndiye aliupa jina, nilikuwa nimeupa jina lingine kabisa, lakini tulipokwenda studio wakati anaweka sauti akaniambia huu wimbo uitwe Jike Shupa, sikubisha.”

Nuh ambaye mke wake amejifungua hivi karibuni, anaendelea kuzungumza kwa kusema halikuwa jambo rahisi kwake kuoa kwani alipita kwenye wakati mgumu sana.

“Kila mtu alifi kiri kuwa nitamuoa Shilole kutokana na ukaribu wetu, ni kweli tulipendana na mwenzangu alikuwa tayari kubadili dini ili tufunge ndoa ya Kikristo, lakini ndiyo hivyo Mungu hakupenda, nikamuoa Nawal.

“Kumuoa huyu binti, dah! (anacheka) ilikuwa kazi ngumu sana, lakini mimi nitumike kama njia ya kuwashauri vijana wenzangu kuwa siyo kila mwanamke unaweza kumchezea chezea, wengine utalazimika kumuona tu.

“Tazama, mimi ni Mkristo safi  kama nilivyosema hapo awali, baba mpiga kinanda, mama mwimba kwaya, lakini nimebadilisha dini kwa sasa mimi ni Muislam kwa ajili ya mke wangu (anacheka tena).

“Huyu bibie katika uhusiano wetu alipata mimba kabla ya ndoa, sasa nilikula mikwara sana, wazazi wake ni Waarabu, baba yake alijua kuwa mimi ni mwanamuziki, ukweli ni kwamba alinitisha, ndugu zake wakanitisha hata mambo mengine siwezi kuyasema sasa, mpaka wazazi wangu wakanionea huruma na kuniruhusu kumuoa Kiislamu, nilibadilishwa jina nikaitwa Nurdin,” anasema staa huyo na kuendelea.

“Lakini maisha ya sasa najua mwenyewe, kama nakwenda msikitini au kanisani kwa kuwa hakuna anayenifuatilia ingawa nina mke wangu ndani na maisha yetu yanakwenda vizuri sana kama unavyoona nimemtuma dogo pampers kwa ajili ya mwanangu mwenye wiki mbili sasa.”

Kuhusu Shilole mara kwa mara kudaiwa kuwa na uhusiano naye wakati tayari ana ndoa yake, Nuh anakanusha hilo na kusema kuwa yeye na msanii huyo wanafanya kazi tu kwa sasa, lakini mapenzi hakuna.

“Unajua hata mke wangu mwanzoni alikuwa akifi kiri kuwa naweza kuwa na uhusiano na Shilole hadi akawa anakuja kwenye kila shoo ninayofanya, lakini baadaye alielewa kuwa ni uhusiano wa muziki tu.

“Waandaaji wengi wa shoo wanaamini kuwa wakiniweka na Shilole wanapata watu wengi, sasa nami nataka mkwanja siwezi kugoma kwenda sehemu alipo, lakini tukishamaliza shoo kila mtu na hamsini zake, hakuna uhusiano wa kimapenzi tena, ile ilikuwa zamani,” anasema Nuh anayemiliki studio ya Last Bon Records.

Comments are closed.