The House of Favourite Newspapers

Mpenzi Wangu Sarafina-09

0

Uzuri wa Gloria ulikuwa balaa, David alikuwa na mawazo tele, kila alipokaa alimfikiria msichana huyo mrembo. Alikuwa mtoto wa kishua, baba yake, Mzee Mpobela alikuwa mfanyabiashara mkubwa nchini Tanzania, alikuwa na makampuni mengi, maduka makubwa, migodi ya dhahabu na vitu vingine vingi.

David alilijua hilo, alihakikisha kwamba anamchukua msichana huyo ili maisha yake yawe laini, apate afueni ya maisha kwani kama kuchunwa na wanawake, alichunwa vilivyo na aliona huo ndiyo muda wa yeye kula pesa za msichana.

Walikuwa wakiwasiliana kama marafiki, David hakutaka kukaa sana kwenye mawasiliano ya kirafiki kitu kilichomfanya kuanza kumchombeza msichana huyo kwa maneno matamu, kwamba alikuwa mzuri kiasi kwamba hata Mungu alikuwa akijivunia kumuumba msichana mzuri kama yeye.

“Hukutakiwa kuwa binadamu, wewe ulitakiwa kuwa malaika,” alisema David, alikuwa akizungumza na msichana huyo ana kwa ana.

“Kweli?”
“Ndiyo! Gloria, nimeona warembo wengi, weupe, weusi, warefu na wafupi, ila kwako! Huna kasoro, wewe ni mrembo uliyekamilika,” alisema David huku akimwangalia Gloria machoni.

Alizaliwa kwenye familia ya kitajiri, alipata kila kitu alichokihitaji ila katika maisha yake alikosa kitu kimoja tu, kusifiwa na mwanaume. Kila mtu aliyemtaka, hasa watoto wa mabilionea wengine, walimfuata, walimpeleka klabu na baada ya kutoka huko wakawa wanafanya mapenzi bila kutongozwa.

Hayo yalikuwa maisha yake, hakuwahi kuambiwa kwamba alikuwa mrembo, hakuwahi kuambiwa kwamba alikuwa na tabasamu pana. Maneno yote hayo aliambiwa na David, ndiyo maneno yaliyomfanya kujisikia kwamba alikuwa mwanamke mrembo, mwenye sifa za kimalaika.

Gloria akajiweka mikononi mwa David, akatokea kumpenda mwanaume huyo kiasi kwamba kwake alikuwa haoni hasikii, haambiwi chochote kile. Hakutaka kujificha, kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia David alionekana kuwa kijana muoaji hivyo kumwambia baba yake na ndugu zake kwamba alipata mwanaume ambaye alistahili kuwa mume wake wa ndoa.

“Una uhakika anakupenda kweli?” aliuliza Mzee Mpobela huku akimwangalia Gloria.

“Ndiyo baba!”
“Narudia tena! Una uhakika anakupenda kweli?” aliuliza mzee huyo.

“Ndiyo baba!”

“Tunahitaji kumuona!”

Hilo halikuwa tatizo, haraka sana Gloria akawasiliana na David na kumwambia kwamba baba yake alitaka kumuona. Alilitegemea hilo, hakutaka kumdanganya Gloria kwani aliamini kupitia msichana huyo angepata kiasi kikubwa cha pesa na maisha yake kubadilika kabisa.

Akamwambia kwamba hilo lingewezekana na hivyo siku iliyofika kwenda nyumbani kwa kina Gloria. Mzee Mpobela alipomuona, akafurahi, alitamani sana kumuona binti yake akiwa na furaha kwani ndiye alikuwa mtoto pekee wa kike mbali na watoto wawili wa kiume aliokuwa nao.

Akakaribishwa ndani ya nyumba hiyo, akaambiwa chochote ambacho angekihitaji angepewa ila alitakiwa kumuheshimu sana Gloria kwani ndiye alikuwa mwanamke aliyemfanya kuwa pale alipokuwa.

“Haina shida baba. Lengo langu ni kumuoa Gloria! Hakuna kingine,” alisema David.

“Tunatoa baraka zote!” alisema mama yake Gloria.

Uhusiano ukawa wazi, David alifurahi kwani kile alichokuwa akikihitaji kilikuwa kimetimia. Kwa kuwa alimaliza chuo na hakuwa na kazi, akapewa kiasi cha fedha cha milioni kumi na kuambiwa kuanza kufanya biashara na kiasi kingine angepewa ndani ya siku chache.

“Nashukuru sana! Nitafanya biashara nyingi kweli,” alisema David huku akikenua, kitendo cha kuwa na Gloria kilimuonyesha maisha mazuri, ila hakujua kitendo cha kuwa na Gloria, kwa upande wa pili kilimuonyesha mwanzo wa maisha yaliyojaa mateso makubwa.

****

Daktari akatoka ndani ya chumba kile, akamkuta nesi wake akilia na Sarafina. Hakujua ni kitu gani kilitokea mpaka wawili hao kulia namna hiyo. Hata kabla hajauliza kitu chochote kile, akachukua koti lake refu na kisha kumvisha Sarafina aliyekuwa na nguo ya ndani pamoja na sidiria.

Akamuuliza nesi kilichokuwa kikimliza na majibu yake ni kwamba aliumia sana jinsi mtoto Malaika alivyokuwa akiumwa. Hakutegemea kumuona mtoto aliyekuwa akiumwa namna ile na wakati mama yake hakuwa na uwezo wowote ule.

Moyo wake ulichoma kupita kawaida, hakuendelea kubaki mahali hapo, akaondoka kwenda nje huku akianza kulia kwa kilio cha kwikwi. Daktari akamchukua Sarafina na kuelekea naye katika ofisi yake, huko, akamwambia kilichokuwa kimetokea kwamba mtoto wake alikuwa kwenye hali mbaya japokuwa wao kama madaktari walikuwa wakipambana kumtibu kama kawaida.

“Anasumbuliwa na degedege na ndiyo maana hali yake imekuwa mbaya namna ile,” alisema daktari huku akimwangalia Sarafina.

“Atapona?” aliuliza kwa sauti ya chini.

“Atapona. Umetokea wapi?”

“Ilala! Nilikuwa mitaani tu!”

“Umetoka Ilala mpaka huku?”
“Ndiyo! Kwa miguu! Dokta! Naomba unisaidie mtoto wangu apone,” alisema

“Mbona hukumpeleka hata Magomeni?”

“Sipafahamu! Ninapafahamu hapa na Muhimbili tu! Sikukaa sana Dar es Salaam dokta. Naomba umsaidie binti wangu,” alisema Sarafina na kuanza kulia mahali hapo.

Moyo wake ulimuuma, ulichoma, alihisi kabisa kitu chenye ncha kali kikimchoma moyoni. Aliendelea kubaki hospitalini hapo, dokta yule aliendelea kumtibu Malaika. Hakukuwa na aliyelala, kila mmoja alikuwa macho.

Yule mwanaume aliyemsaidia hakutaka kuendelea kubaki hospitalini hapo, akaondoka huku akiahidi kumtembelea tena mapema siku inayofuata

Moyo wa Sarafina ulimwambia kabisa kwamba mtoto wake hakuwa na muda mwingi wa kuishi, ilikuwa ni lazima afariki dunia kitandani pale. Alimwambia daktari kwamba ingekuwa vizuri kama angepata nafasi ya kwenda kukaa na mtoto wake chumbani mule, pembeni ya kitanda chake kwa ajili ya kufuatilia kila hatua.

Hilo halikuwa tatizo, akaruhusiwa na kuingia ndani. Macho yake yalipotua kwa Malaika, moyo wake ukauma zaidi, kitandani pale alipokuwa amelala alionekana kama mfu, mashine ya kupumulia ilikuwa puani mwake huku dripu ikining’inia juu yake.

Sarafina alilia, aliendelea kuumia, usiku mzima hakuyaruhusu macho yake kufumba, alikesha huku akimwangalia Malaika tu. Alimuomba Mungu pembeni ya kitanda cha mtoto wake, aliamini kwamba angeweza kumpa nafasi nyingine ya kuishi.

“Mungu! Nakuomba umpe nafasi nyingine. Kama umempa nafasi ya kufika hospitali salama, kwa nini usimpe nafasi nyingine ya kuwa na afya tena?” aliuliza Sarafina huku akionekana kuwa na huzuni mno.

Mpaka asubuhi inaingia, bado Malaika alikuwa kwenye hali ileile. Sarafina hakuacha kumuomba Mungu, aliamini kwamba angeweza kumponya mtoto wake. Hali yake haikubadilika lakini ilipofika saa nne asubuhi, mwili wake ukaanza kurudi katika hali ya kawaida, joto la mwili wake likaanza kupungua na mwisho wa siku kuyafumbua macho yake.

Sarafina hakuamini alichokuwa akikiona, akatoka kitini na kupiga magoti chini, akainyanyua mikono yake juu na kumshukuru Mungu. Hakuamini kama alimpa nafasi tena mtoto wake ya kufumbua macho, kwa jinsi alivyokuwa akishukuru mpaka wagonjwa wengine walishangaa.

“Sina mwingine zaidi ya Malaika wangu. Najua nitakufa kwa kansa ya matiti lakini naomba huyu aendelee kuwa kwenye hali yake ya kawaida,” alisema Malaika huku akimwangalia mtoto wake.

Siku hiyo aliendelea kubaki hospitalini hapo, kila alipokuwa akiletewa chakula kwa ajili ya kula, alishindwa, hakuwa na hamu ya kula hata kidogo. Kitu alichokihitaji wakati huo si chakula bali ni afya ya mtoto wake tu.

Madaktari na manesi walimlazimisha kula lakini alikataa, aliwaambia dhahiri kwamba hawezi kula na wakati mtoto wake hakuwa akinywa uji, angejisikia vipi kama mzazi akashiba na mtoto wake kuwa na njaa?

Ilipofika saa moja usiku hali ya Malaika ikaanza kutengemaa kwa nguvu, akarudi katika hali yake ya kawaida, aliendelea kupata nafuu jambo lililomfanya Sarafina kufurahi kwani hakutegemea lile alilokuwa akiliona.

“Hali yake itaendelea kutengemaa, wala usijali!” alisema daktari huku akimwangalia Sarafina.

Sarafina na mtoto wake walikaa hospitalini kwa siku tatu ndipo akaruhusiwa kutoka. Hakuwa na pa kwenda, kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ndivyo ilivyokuwa kipindi hicho, akaanza kulala mitaani huku akiomba misaada katika magari yaliyokuwa yakipita.

Alikuwa kwenye kipindi kigumu mno, aliteseka lakini hakutaka kumuona mtoto wake akitoka mikononi mwake. Walizunguka sehemu kubwa, usiku wa saa nne ulipokuwa ukimkuta ndipo hapohapo alipokuwa akilala.

Maisha hayakubadilika! Alizurura kila kona jijini Dar es Salaam, hakuacha kuomba kwa kila mtu aliyekuwa akikutana naye njiani. Baada ya kupita miezi ndipo akabahatika kukutana na mtu ambaye alikuwa na hamu ya kukutana naye.

Siku hiyo, alinyeshewa sana na mvua, alikuwa amelowa, hakuwa na kitu, hakutaka kupumzika kwani tangu asubuhi mpaka muda huo ndiyo kwanza alipata shilingi elfu tano. Alijifunika khanga huku akiyafuata magari mbalimbali yaliyokuwa yamepanga foleni.

Wakati akiwa amelifuata gari moja la kifahari kwa lengo la kuomba, dirisha la gari likafunguliwa na msichana mmoja mrembo, aliyependeza kupita kawaida. Msichana huyo akamwangalia Sarafina, alimuonea huruma, alionekana kuteseka, mvua ilimpiga na alikuwa amemfunika Malaika kwa khanga yake ambayo haikuifanya kumzuia na maji ya mvua, aliendelea kulowa.

“Pole sana,” alisema msichana huyo huku akimwangalia Sarafina, dereva wa gari hilo alitulia, umakini wake ulikuwa mbele, alionekana kukasirika na foleni iliyokuwa ikimkabili.

“Nashukuru!”

“Mtoto wako mzuri! Anaitwa nani?” aliuliza msichana huyo.

“Malaika!”
“Ooh! Jina linaendana na yeye mwenyewe. Pole kwa mvua. Shika hii!” alisema msichana huyo huku akiingiza mkono kwenye mfuko wa kaki uliokuwa na noti nyingi kisha kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini na kumpa.

“Nashukuru! Nashukuru sana mama! Nashukuru sana,” alisema Sarafina huku akianza kupiga magoti, hakujali mahali alipokuwa, hakujali kama mvua ilikuwa ikinyesha sana, alichokuwa akikihitaji ni kumuonyeshea shukrani msichana huyo ambaye kwa msaada wake, na umri wake mdogo alimuita jina la mama kabisa.

“Usijali!”

Wakati wawili hao wakizungumza, macho ya Sarafina yakatua kwa mwanaume aliyekuwa akiendesha gari hilo. Alimwangalia vizuri, alikuwa David, mwanaume aliyewahi kutembea naye, akampa mimba na kisha kumuacha.

Hakutoa macho yake kwa David, aliendelea kumwangalia huku akiwa haamini kama kweli huyo alikuwa David au mwanaume mwingine aliyefanana naye kiasi kile.

“David…!” aliita Sarafina, David akashtuka, akamwangalia mtu aliyemuita, macho yake yakagongana na Sarafina, akasikia moyo wake ukipiga paaa! Hakuamini alichokuwa akikiangalia, mbaya zaidi, alipoyapeleka macho yake kwa mtoto aliyebebwa na Sarafina, alifanana na yeye kwa kiasi kikubwa, alionekana mtoto mwenye njaa, alikuwa mwembamba mno kiasi kwamba unaweza kuhisi kwamba muda wowote ule angekufa.

“David…ni wewe?” aliuliza Sarafina lakini hata kabla mwanaume huyo hajajibu, foleni ziliruhusiwa, kwa haraka sana David akapiga gia, hakuzungumza kitu, akaliondoa gari mahali hapo na kumuacha Sarafina akiwa haamini alichokiona, akabaki akiwa amesimama, akitetemeka kwa baridi kali huku mvua ikiendelea kunyesha.

“Mungu wangu! David ameniacha, hakutaka hata kunisikiliza? Anakula maisha na mwanamke mwingine huku mtoto wake akiteseka?” alijiuliza Sarafina huku akilia, kile alichokiona, hakuamini kabisa.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

Leave A Reply