The House of Favourite Newspapers

Yanga Yapewa Mchongo Wa Kuifunga Simba

Kikosi cha timu ya Yanga.

YANGA na timu nyingine za Ligi Kuu Bara zimepewa bonge la mchongo kwamba, kama zinataka kuifunga Simba basi kazi wanayotakiwa kuifanya ni kumzuia kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude.

 

Aliyetoa mchongo ni Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche ambaye timu yake Jumatano wiki hii, ilifungwa bao 1-0 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana tena kwenye Uwanja wa Taifa, Aprili 7, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa pili baada ya mzunguko wa kwanza kutoka sare ya bao 1-1.

 

Hadi sasa Yanga imeachwa pointi saba na Simba iliyo kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 41 huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 17. Moja kati ya mahali pa Yanga kupunguza tofauti hiyo ya pointi ni katika mchezo kati yao.

 

Cheche alisema timu yoyote inayotaka kuifunga Simba kwa sasa ni lazima ihakikishe inamzuia Mkude tu kwani ndiye kila kitu kwa timu yake.

 

“Kama ukitaka kuifunga Simba ni rahisi sana, mzuie Mkude tu kwa maana ya kutompa nafasi ya kucheza mpira, kwani yeye ni mchezaji mwenye madhara pekee kwa wapinzani.

 

“Sisi wenyewe tulifanya uzembe kwani wachezaji wetu walishindwa kucheza kwa maelekezo ambayo tumewapa kwa kushindwa kumzuia Mkude,” alisema Cheche.

Aliongeza, kabla ya mechi hiyo na Simba waliwapa maelekezo wachezaji wao jinsi ya kuwazuia wachezaji wenye madhara kwenye kikosi cha Simba akiwemo Mkude na Emmanuel Okwi aliyewafunga bao pekee.

Comments are closed.