The House of Favourite Newspapers

Uchunguzi Wamrudisha Aveva Muhimbili, Malinzi Apata Ahueni

Rais wa Simba, Evans Aveva (kulia) makamu wake wa rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.

RAIS wa Simba, Evans Aveva, jana alishindwa kuhudhuria mahakamani katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili kwa mara ya nne mfululizo kutokana na hali yake kutoimarika, badala yake alirudishwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili uchunguzi wa afya yake.

 

Aveva anakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha kiasi cha dola 300,000 za Kimarekani akiwa na makamu wake wa rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.

 

Kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama ya Kisutu, Victoria Nongwa, ambapo Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Leonard Swai aliiambia mahakama hiyo kuwa tayari wamekamilisha uchunguzi wa kesi hiyo na jalada limerudishwa tena kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

 

Swai alisema kuwa wameshindwa kumfikisha tena mahakamani mtuhumiwa namba moja, Aveva kwa kuwa alikuwa amepelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

 

Kufuatia kauli ya Swai, aliomba tarehe nyingine ili waweze kufuatilia jalada kwa DPP kauli ambayo iliungwa mkono na mawakili wa utetezi ambao ulikuwa ukiongozwa na Stephen Ally kabla ya hakimu Nongwa kusogeza mbele kesi hiyo hadi Machi Mosi, mwaka huu.

 

Kwa upande wa kesi ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake ambayo nayo imesogezwa mbele kufuatia Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP kuomba muda zaidi ili aweze kulipitia kwa umakini jalada hilo kabla ya kufanya maamuzi.

 

Malinzi anashitakiwa kwa makosa ya kughushi nyaraka zikiwemo risiti 20 za TFF pamoja na shitaka la utakatishaji fedha kiasi cha dola za Kimarekani 375,418 akiwa na washitakiwa wengine ambao ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Nsiande Mwanga ambaye alikuwa mhasibu wa shirikisho hilo.

 

Katika kesi hiyo iliyoitwa jana kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Wilbad Mashauri ambapo Mwendesha mashitaka Mkuu wa upande wa Takukuru Leonard Swai aliiambia mahakama hiyo kuwa bado jalada la kesi hiyo limekwama kwa DPP hivyo wanaendelea kulifuatilia.

 

Hoja hiyo ilionekana kupingwa na mawakili wa upande wa utetezi waliokuwa wakiongozwa na Abraham Senguji ambao waliomba mahakama hiyo ihakikishe inapanga siku za karibu ili kuwaongezea presha upande wa mashitaka kwa kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa jalada hilo kwa DPP kwani wateja wao wanaendelea kuteseka mahabusu kwa muda mrefu.

 

Kutokana na hoja hiyo ya upande wa mawakili wa utetezi, hakimu Mashauri ameisogeza mbele kesi hiyo hadi Machi Mosi, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa tena.

Comments are closed.