The House of Favourite Newspapers

ROMA AWAFUNGUKIA WANAOFELISHWA NA NDOA

Related image
Ibrahimu Musa ‘Roma Mkatoliki’,Akiwa na Mkewe

ALIINGIZA somo la ‘Mathematic’ kwenye ulimwengu wa Muziki wa Hip Hop, mashabiki wakaingia ‘class’ kupiga msuli, akawaita ‘Wanakondoo’ kisha akajitangaza kwamba ndiye ‘Mr. President’ wa ‘Tanzania’ mwaka ‘2030’, kila mtu akamtakia kheri na kumwambia Viva R.o.m.a, lakini baadaye akadai kwamba alikuwa anatania na nia yake ni kwenda kuishi Zimbwabwe!

Hilo likawa gumzo kila kona mtaani, kuliko hata tukio lake la kutekwa, lakini mambo yalipoa baada ya kusema kwamba Zimbabwe alikuwa anakwenda kupiga ‘Mechi za Ugenini’.

Watu wakalipuka ‘aaaaah mbona Roma unatuzingua’, warembo wakaibuka na kusema aachwe kwani ni Mwanaume Mashine, lakini wengine wakaibuka na kudai ni Kibamia, ndiyo maana hakumuweza hata Maua Sama.

Unaweza kuwa unajiuliza ninazungumzia nini hapa, ha! ha! haa! Kama nimekuacha ninazungumzia nyimbo mbalimbali ambazo zimemuweka mwanamuziki Ibrahimu Musa ‘Roma Mkatoliki’, hapo alipo kwenye gemu la Muziki wa Hip Hop.

Sina shaka kwamba Roma, ambaye anajiandaa kuangusha shoo ya kibabe Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live, uliyopo Mbagala Zakhem na wakali wengine akiwemo Juma Nature na Msaga Sumu, unampenda na unamkubali.

Mbali na kumkubali pia kuna mengi unapenda kuyasikia kutoka kwake, huyu hapa anakata kiu yako kwenye mahojiano na Showbiz Xtra, twende pamoja!

Showbiz: Unajiandaa kupiga shoo Dar Live, Jumapili, una kipi cha kuwaeleza mashabiki wako?

Roma: Wanafahamu ninachofanya ninapokuwa mbele yao, wasikose kufika Dar Live, tamasha hili ni zaidi ya matamasha yote waliyowahi kunishuhudia.

Showbiz: Tukirudi kwenye kazi zako, wewe ni mwanamuziki mkubwa ambaye unasikika ndani na nje ya Bongo, inakuwaje huna menejimenti?

Roma: Nafikiri ni kwa sababu mambo mengi ninaweza kuyamudu mwenyewe, pamoja na watu wangu wa karibu ambao ninashirikiana nao. Hao kwangu ni kama menejimenti lakini kwa uhalisia ni familia yangu kwenye muziki. Kwa hiyo sikosi kitu, kwa kutokuwa na hiyo menejimenti.

Showbiz: Unafikiri kwa nini muziki wa Bongo Fleva, umekwenda mbali zaidi kwa sasa kuliko muziki wa Hip Hop?

Roma: Mimi ninaamini aina zote za muziki zimekwenda mbali. Lakini kama unavyosema Bongo Fleva ipo mbali zaidi, pengine ni kwa sababu ni muziki ambao watu wanaweza kucheza bila hata kuelewa kile kilichoimbwa.Related image

Tofauti na Hip Hop, ni lazima uwaguse watu kwa mashairi yako na mambo mengine.

Showbiz: Sasa mnashindwaje kuwagusa watu?

Roma: Pengine lugha inaweza kuwa changamoto. Wanamuziki wengi tunaimba Kiswahili tu, kwa hiyo wengi tunaowagusa ni wale wanaosikiliza Kiswahili.

Showbiz: Tukiangalia Joh Makini alijaribu kutoboa anga mpaka akawa anasikilizwa zaidi Nigeria kwa kuimba Kiswahili, Darasa pia lakini kuna wanamuziki wakali Afrika kama Cassper Nyovest na Sarkodie wanaimba sana kwa lugha za nyumbani kwao lakini wanaeleweka, unawezaje kusema Kiswahili ni tatizo?

Roma: Binafsi ninaona hivyo! Lakini hapohapo kwa ulichosema ninakubali pia menejimenti ni changamoto. Unajua ukiangalia timu ya Cassper inayosimamia kazi zake, ukiiona tu unajua ni watu siriazi ambao kila mmoja anafaidika na kazi zetu.

Sisi mara nyingi unakuta tunachokipata hakijitoshelezi kuajiri watu wa kusimamia kazi zetu.

Showbiz: Una miaka minne sasa kwenye ndoa, ni changamoto gani ambazo unakutana nazo kwenye kazi?

Roma: Changamoto ni nyingi, lakini ili kuziepuka wakati wa kazi huwa ninaacha mambo ya ndoa pembeni na kupiga kazi. Siwezi kuacha kukesha studio kwa sababu ya ndoa. Siwezi kuacha kupiga shoo kwa sababu ya ndoa. Kwa hiyo watu wengi waliofeli kisa ndoa, hapa nitaweka wazi kwamba walishindwa kumentaini hapo. Katika maelewano na watu wao wa karibu hasa kwenye kazi zao.

Wake wanashindwa kuwaelewa wanaume wao na kuwaacha wafanye kazi kama ilivyokuwa awali kabla ya kuwa nao. Hapo ndipo inapokuwa tatizo. Lakini kwa upande wangu mke wangu ni muelewa sana!

Showbiz: Jambo la mwisho la kumalizia kwa leo.

Roma: Yapo mengi lakini leo nimalize na hili kla Dar Live pekee. Watu wasikose Dar Live, moto utawaka

Comments are closed.