The House of Favourite Newspapers

BINGWA WA ENGLAND NI MAN CITY

BAADA ya mechi mbili za Ligi Kuu England kupigwa, tayari picha ya mwanzo ya ligi hiyo msimu huu wa 2018/2019, imeanza kuonekana huku baadhi ya timu zikiwa hazina uwezo wa juu sana na nyingine zikionyesha kasi.

 

Huu ni msimu ambao mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kufahamu ni timu gani inaweza kutwaa ubingwa tena baada ya msimu uliopigwa ubingwa huo kutwaliwa na Man City.

 

Kabla ligi haijaanza timu kadhaa zilikuwa zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Liverpool na Tottenham Hotspur ndiyo zilikuwa zinapewa nafasi kubwa sana.

Lakini taratibu mambo yameanza kuwa tofauti na timu mbili kati ya hizo zimeshapoteza michezo yao, Arsenal wamepoteza michezo miwili ya mwanzoni.

 

Lakini pia Manchester United nayo imepoteza mchezo mmoja kwenye ligi hiyo, lakini ikionekana kuwa inapigwa vita sana kwa kuwa imepoteza dhidi ya timu ndogo sana ya Brighton.

 

Pamoja na kwamba wengi wanaweza kuwa na mitazamo yao, lakini kwa uzoefu wangu kwenye Ligi Kuu England na jinsi nilivyotazama vikosi vyote naamini kuwa bado klabu ya Manchester City ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

City pamoja na kushinda michezo yao miwili, mchezo wa kwanza dhidi ya Arsenal waliposhinda mabao 2-0 na mechi iliyofuata dhidi ya Hundelisfield walipapata ushindi wa mabao 6-1, wanaonekana kuwa timu iliyojipanga vizuri zaidi kuliko nyingine zote kwenye ligi hiyo.

 

Wengi wamekuwa wakitumia rekodi na kusema kuwa haijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni timu kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo, lakini inaonekana kuwa City msimu huu wanaweza kuvunja mwiko huo.

Ufiti wa mshambuliaji wao, Sergio kun Aguero, uwepo wa kiungo David de Bruyne ambaye kwa sasa anasumbuliwa na majeraha na kitendo cha kocha wa timu hiyo kumsajili Riyard Mahrez, kinaonyesha kuwa timu hii inaweza kuitikisa timu yoyote.

 

Kasi ya Manchester City kwenye mchezo dhidi ya Arsenal ilionyesha kuwa hii ni timu iliyojipanga vyema kwa ajili ya kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili na ina uwezo wa kufanya hivyo.

 

Pamoja na kutwaa ubingwa huo, pia itaruhusu mabao machache sana kwa msimu huu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Nafasi ya pili kwenye ligi hiyo hakika itakwenda kwa Liverpool, wengi wanaweza wasikubaliane na hili lakini ukweli ni kwamba kama Liverpool wataweza kukitumia kikosi chao vizuri, lazima watakuwa kwenye nafasi hii au wasubiri Man City wadondoke wao watwae ubingwa.

 

Liverpool pamoja na kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Timu hii ilikosa baadhi ya vitu msimu uliopita, lakini mojawapo ilikuwa ni kutokuwa na kipa mwenye uwezo wa juu, lakini kwa sasa kitendo cha kumsajili kipa Allision na kiungo Nabil Keita kinaonyesha kuwa timu hiyo kwa sasa itakuwa imara zaidi.

 

Moja ya safu ya ushambuliaji ambayo inaweza kufanya mambo makubwa

sana kwenye ligi hiyo kwa msimu huu ni ile ya Liverpool ambayo itakuwa na Saidio Mane, Mohammed Salah na Roberto Firimino, ambao wanaaminika kuwa watakuwa moto mkali.

 

Nafasi ya tatu, Manchester United, huwezi kuita United kwenye kasi ya Ligi Kuu England hata kama imepoteza mchezo mmoja hadi sasa.

 

Kikosi hiki chini ya kocha Jose Mourinho hakikufanya usajili mkubwa sana, lakini uwepo wa mastaa kama Romelu Lukaku, Fred na Marcus Rashford wanaweza kuisaidia timu hiyo kufanya makubwa msimu ujao.

 

Hofu kubwa ya United inaonekana kuwa kwenye safu ya ulinzi ambayo inaonekana kutokuwa tofauti sana na ile ya msimu uliopita.

Kosa lingine ambalo linaweza kuwakwamisha United ni kitendo cha kocha wa timu hiyo, kulalamika kila mara kuwa hakupewa fedha za kutosha za usajili.

 

Nafasi ya nne, Arsenal na Chelsea, hapa kuna timu

mbili zitakuwa zinawania nafasi hii, mashabiki wa Arsenal wanaweza kukubaliana na hili, lakini itakuwa ngumu kwa wale wa Chelsea.

Chelsea ambayo iliichapa Arsenal mabao 3-2, bado inaonekana kuwa itakuwa timu bora kuliko ile ya msimu uliopita ambayo ilimaliza kwenye nafasi ya tano.

 

Lakini itakuwa na wakati mgumu wa kumaliza juu ya nafasi ya nne kutokana na kuwa na safu ya kawaida sana ya ulinzi na kiungo, lakini hata safu yao ya ushambuliaji haiwezi kuwa na uwezo wa kuipa timu hiyo ubingwa.

 

Arsenal itakuwa ileile pamoja na kwamba imemaliza msimu uliopita ikiwa nje ya nne bora, tayari imeshapoteza michezo miwili, endapo ikipoteza michezo mingine miwili itakuwa imetoka kwenye kasi za ubingwa wa Ligi Kuu England rasmi.

 

Hofu kubwa ya Arsenal ni wachezaji wengi kwenye safu ya ulinzi kuwa wageni na hivyo itawachukua muda mrefu kuelewana, hata hivyo tayari safu hiyo imesharuhusu mabao matano kwenye michezo miwili.

Comments are closed.