The House of Favourite Newspapers

Kama Umeajiriwa, Makala Hii Inakuhusu Sana!

NI wiki nyingine tulivu kabisa, tunakutana kupitia safu hii; ambayo tunaelimishana na kukumbushana mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kila siku.

 

Ni safu inayokuhusu wewe. Hivyo, kama una lolote ambalo linakusumbua kwenye maisha yako, usisite kunitafuta kupitia namba zangu zilizopo hapo juu ili tuzungumze na kushauriana kirafiki zaidi.

 

Mpenzi msomaji wangu, kazi ni kitu cha msingi sana katika maisha ya binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba bila kufanya kazi, maisha yako yatakuwa magumu na hakika utakuwa tegemezi katika jamii unayoishi.

 

Ndiyo maana leo hii, kila mmoja wetu anapambana kuhakikisha anafanya kazi; aidha ya kujiajiri ama ya kuajiriwa, ili mradi mwisho wa siku ajiingizie kipato ambacho kitamsaidia katika kuyaendesha maisha yake.

 

Wakati mwingine haipo hivyo, wapo watu ambao wanafanya kazi lakini ukiwafuatilia sana utagundua hakuna faida wanayoipata kupitia kazi wanayoifanya.

Ni kweli kwamba kazi ni heshima, unapopata ile nafasi ya kutoka asubuhi na kwenda kazini, unakuwa na utofauti na yule ambaye hajui kesho aende wapi wala afanye nini ili kujipatia kipato. Wewe unakuwa na heshima ya kwamba jamaa ni mfanyakazi.

 

Swali la kujiuliza sasa ni kwamba; je, kipato unachopata kupitia kazi unayofanya kinaboresha maisha yako? Je, kuna tofauti kati yako na wale ambao wako kijijini wakiwa hawana hili wala lile, lakini wanakula na kulala?

 

Nasema hivyo kwa sababu, utakuwa ni mtu wa ajabu sana kama utakuwa unafanya kazi ili upate tu pesa ya kula na kulipia pango. Kwamba kila ukipata mshahara unaishia kwenye kulipia madeni, kulipia kodi kisha unaanza moja.

 

Au unafanya kazi, lakini bado kula na kulala kwako ni shida, yaani unafanya kazi lakini kipato unachopata hakiwezi kukupatia yale mahitaji yako muhimu kisha ukapata ziada ya kufanyia mambo ya kimaendeleo. Badala yake sasa unabaki na ile heshima tu, kwamba unafanya kazi. Sasa utakuwa unafanya kazi au unazuga?

Naandika makala haya nikiwa na mifano ya watu ambao wanafanya kazi iliradi tu wawe na kitu cha kuwaweka bize. Mmoja wa watu hao ni kijana anayeitwa Juma Suleimani wa Mbagala jijini Dar es Salaam.

Huyu anafanya kazi kwenye kiwanda kimoja kilichopo Mikocheni jijini Dar. Mwenyewe anaeleza kuwa, anaishi Mbagala lakini anafanya kazi Mikocheni na mshahara anaopata siyo mkubwa sana kiasi kwamba, akiupokea unaishia kwenye kulipa madeni na pesa inayobaki ni kwa ajili ya kula na kulipa nauli.

 

Hana kitu kingine anachoweza kufanya kupitia mshahara wake, hata kupanga chumba ameshindwa. Lakini ukimuona huwezi kuamini. Yuko smati, amesoma lakini kutokana na maisha ameona aendelea kufanya kazi hiyo licha ya kutoona faida.

 

Huyo ni mmoja wa watu ambao wanafanya kazi lakini bado maisha yao ni magumu. Kweli Wazungu wanasema; ‘Something is better than nothing’ kwamba kitu hata kama ni kidogo ni bora kuliko kutopata kitu kabisa. Yaani ni bora ukawa unafanya kazi hata kama haikuingizii kipato kikubwa kuliko kukaa nyumbani na kuwa tegemezi.

 

Sipingani na dhana hiyo, lakini ukweli ulio wazi kabisa ni kwamba wapo watu ambao wanafanya kazi lakini bado maisha yao ni duni. Unamuona kila siku anakwenda kazini lakini akiumwa anashindwa kupata hata pesa ya kununulia dawa. Faida ya kufanya kazi iko wapi?

 

Kama unaona unafanya kazi lakini huoni dalili ya kazi hiyo kukupa mafanikio, bora uachane nayo na uangalie kitu kingine cha kufanya. Kama uko mjini na kazi unayofanya, ni kama unatwanga maji kwenye kinu. Heri urudi kijijini ukalime kuliko kubaki mjini halafu ikotokea kwenu kuna tatizo, hata nauli unakopa.

 

Ninachokushauri wewe msomaji wangu ni kufanya tathimini ya kazi unayofanya. Je, ina mchango wowote katika kuyaboresha maisha yako? Jiulize umeifanya kwa muda gani na imekubadilisha? Majibu utakayopata ni vyema ukayafanyia kazi.

Comments are closed.