The House of Favourite Newspapers

KIJIJI AMBAKO WANAWAKE NDIYO HULIPA MAHARI!

Katika kijiji cha Nyamashekhe kilochopo mkoa wa magharibi nchini Rwanda kumekithiri utamaduni wa wanawake kulipa pesa kwa mwanaume ili  waolewe. 

Mtindo huo mpya wa maisha umezua gumzo katika jamii huku baadhi ya watu wakihoji hatima ya siku zijazo za utamaduni wa kulipa mahari. BBC imetembelea kijiji hicho na kuzungumza na wanawake, wanaume, viongozi wa kijiji na baadhi ya wahusika ili kufahamu zaidi kwa nini utamaduni huo unazidi kupata umaarufu.

Kaitesi Lilian mmoja wa kina mama wa kijiji hicho anasema: “Mvulana anapokuja kumposa msichana wako unajua kwamba mambo yameiva, lakini ndoa ikikaribia unasikia kwamba amemgeuka na kumwambia kwamba ndoa haitawezekana ikiwa hatapewa pesa za mahari”.

Image result for rwanda

Alipoulizwa mbona wanawake wengine wameolewa bila kufuata utaratibu huo, alifafanua kwa kusema:”Wakati huo binti alikuja na kuangua kilio huku akinishinikiza niuze kila kitu hata mabati au shamba ilimradi yeye apate pesa ya kumpa mchumba wake.”

Tofauti na maeneo mengine ya nchi ambapo mwanaume ndiye hutoa posa kwa familia ya mwanamke, utamaduni huu mpya unawashinikiza wasichana kumlipa pesa mwanamume.  Inasadikiwa kuwa pesa hizo ni kama Dola 1500 (Sh. milioni 3.4) na huongezeka kulingana na uwezo wa familia ya msichana. Walioshuhudia wanasema pesa hizo lazima zipatikane kwa udi na uvumba.

Katika tamaduni za Wanyarwanda mahari lazima itolewe tena na bwana harusi mtarajiwa. Hata kama mahari haijakamilika kwa wakati huo familia husika zinakubaliana jinsi itakavyolipwa, na hatimaye harusi hufanyika. Katika mkoa wa msgharibi nchini Rwanda pesa hizo zikikosekana hakuna harusi tena.

Kaibanda Bernard ameiambia BBC kuwa: “Vijana wanafanya hivyo wakisema idadi ya wasichana sasa hivi ni kubwa sana.  Wasichana wengine wameshindwa kuvumilia, ambapo msichana akitinga umri wa miaka kumi na tano hivi anatafuta pesa kwa nguvu ili aweze kumnunua bwana. Vijana wenyewe wanaona ni ishara ya ushirikiano katika familia mpya kutokana na hali ya maisha ilivyo ghali siku hizi.

John Gatera anasema mmoja wa watu wanaounga mkono mtindo huo wa maisha anasema: “Zamani kutoa mahari ilikuwa ni kitu rahisi sana, ni ngombe labda na kiwanja lakini sasa hata kupalilia sehemu ya ujenzi lazima ulipe pesa”.

Anasema yeye binafsi akifikisha umri wa kuoa lazima msichana amlipe pesa la sivyo harusi haitafanyika. Baadhi ya watu katika kijiji cha Nyamashekhe wanataka serikali kuingilia kati suala hilo. Mmoja wao ni mzee Kaihura ambaye anasema: ”Kijana hawezi kupata heshima katika jamii ikiwa hatatoa mahari”.

Utamaduni huu mpya umepokelewaje?

  • Wazazi walio na mabinti waliofikisha umri wa kuolewa wana wasiwasi huenda mtindo huo mpya wa maisha ukaenea kote nchini ikiwa hatua hazitachukuliwa kuukomesha.
  • Pia wanahofia suala hili huenda likabadilisha kabisha utamaduni wa jadi wa wanaume kulipa mahari.
  • Vijana, hususan, katika mkoa huo wanadaiwa kujiona ”mastaa”, hali ambayo huenda ikawafanya kuzembea majukumu yao ya familia hata wakifanikiwa kupata wake zao.

Si mara ya kwanza mkoa huo wa Magharibi ambao ndiyo mkubwa kuliko mikoa mingine, kuzua gumzo kuhusiana na masuala ya kijamii.

Kabla ya mtindo huu wa sasa wa vijana kutaka walipwe pesa na wasichana ili wawaoe, kulikuwa na wakati inadaiwa kuwa mvulana akimtembelea mchumba wake kwao sharti achinjiwe kuku.

Comments are closed.