The House of Favourite Newspapers

AJALI ILIYOUA MSANII NA WENZAKE WATATU… UNDANI NI HUU!

JUMAMOSI iliyopita, msanii wa muziki wa uswazi Mchiriku, Jackson Simela ‘Dogo Jack’(pichani) na wenzake watano walipata ajali ya gari na kufariki dunia papo hapo maeneo ya Nanenane mkoani Morogoro, Risasi Mchanganyiko linakupa undani zaidi wa tukio hilo.  

 

Kwenye ajali hiyo iliyotokea jirani na Kituo cha Mafuta cha Nanenane, Dogo Jack alikuwa na wenzake 6 wakielekea makaburini kumzika ndugu wa msanii huyo aitwaye Elizabeth Kazimoto ndipo walipogongana uso kwa uso na lori aina ya Scania.

 

Mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Chopa Ally, alisema kwa jinsi alivyoshuhudia ajali hiyo ilitokana na uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari dogo alilokuwemo marehemu Dogo Jack.

 

“Naweza kusema ajali hii imetokana na uzembe wa dereva wa hii gari dogo, akiwa mwendokasi huku mbele yake lori lilikuwa kasi, huyu dereva wa gari dogo aliyekuwa akitokea Msamvu alikata ghafla akitaka kuingia sheli bila kuchukua tahadhari ambapo lori hili ambalo lilikuwa kwenye saiti yake likitokea upande wa Dar liligongana uso kwa uso na gari hilo dogo.

 

“Watu 6 waliokuwa kwenye hili gari dogo walikufa hapahapa huku majeruhi mmoja (Abdul) akiwa amekimbizwa hospitali baada ya kichwa kufunuka na kuvunjika mguu,” alisema Chopa.

Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Shabani Athuman alipohojiwa na mwandishi wetu eneo la tukio, alidai kwamba dereva wa gari hilo dogo ambaye ni miongoni mwa watu waliokufa aliyemtaja kwa jina moja la Offin, alipewa gari hilo akalioshe na alipomaliza ndipo alipoenda kwenye msiba na kuwababe wenzake 6.

 

“Offin alipewa gari akalioshe baada ya kupata habari mama wa rafiki yake lbrahim amekufa akaamua kwenda kuzika, bahati mbaya wakati wanaingia sheli waongeze mafuta wakagongana uso kwa uso na lori. “Offin na Juma Salum maarufu Allu ambao wanaishi Kilimahewa tumewazika jana (Jumapili iliyopita),”alisema shuhuda huyo. Mwandishi wetu alitinga Kilimahewa na kufanikiwa kuzungumza na baba wa marehemu Juma, Edward Hizza:

 

“Salum ni mwanangu ambaye ni miongoni mwa watu waliokufa wakiwa njiani wakielekea kumzika mama wa rafiki yao,” alisema Hizza ambaye ni mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na timu ya taifa. Baadaye mwanahabari wetu alitinga nyumbani kwa kina Dogo Jack, Mtaa wa Juhudi Zako, Kata ya Mwembesongo na kushuhudia umati wa watu wakiwemo wa wasanii wa singeli, mchiriku kutoka Dar wakiongozwa na Man Fongo.

 

Akihojiwa na Risasi Mchanganyiko, msemaji wa familia hiyo, Dominick Mwimbaje ambaye ni mdogo wake Dogo Jack alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na misiba hiyo: “Desemba 7, shangazi yetu Elizabeth Kazimoto aliyekuwa mgonjwa alifariki dunia na siku iliyofuata yaani Jumamosi Desemba 8 tulienda kumzika Makaburi ya Bigwa.

“Kabla ya kwenda kuzika tuliketi kikao cha familia ambapo tulikubaliana watu 7 waingie kaburini miongoni mwao ni Jack na Ibrahim Salum ambaye ni mtoto wa marehemu Elizabeth. “Tulipofika makaburini MC anasoma majina, Jack na lbrahim hawapo basi tukateuwa watu wengine tukamsitiri shangazi yetu. “Cha ajabu tunafika hapa nyumbani tunaambiwa Jack, lbrahim na wenzao wamepata ajali na wamekufa.

 

“Wakati tunaenda kuzika sisi tulipita barabara ya zamani ya Dar wao pekee wakapita barabara ya sasa ya Dar na kupata ajali hiyo,” alisema  msemaji huyo wa familia.Msemaji huyo wa familia alipoulizwa ni kweli dereva wa gari hilo alipewa akaoshe alijibu. “Kimsingi dereva hatumjui tumeambiwa ni rafiki wa lbrahim hata sisi tumesikia kama ulivyosikia wewe kwamba gari siyo lake alipewa akalioshe lakini kwa urafiki na lbrahim aliamua kuja kuzika,” alisema.

 

Alipotakiwa kutaja watu waliokufa na majeruhi, msemaji huyo wa familia alijibu: “Waliokufa ni lbrahim Salum, Jack Simela, Juma Salum, Amos, John na dereva Offin. Abdul amenusurika ingawa ameumia vibaya kuchwani,” alisema.

Mwandishi wetu alizungumza na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Morogoro (RTO), SSP Michael Stephen ambaye alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo lakini akamuomba mwandishi wetu awasiliane na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa.

 

Hata hivyo, awali Ofisa Habari wa Polisi, Afande Mohamed aliwaambia waandishi wa habari kuwa kamanda angezungumzia tukio hilo Jumatatu (juzi) lakini baadaye akadai kwamba ameahirisha hadi Jumanne (jana) kwani amepata udhuru.

Stori: DUNSTAN SHEKIDELE, MOROGORO

Comments are closed.