The House of Favourite Newspapers

Arusha Utd yajitoa Daraja la Kwanza

BODI ya Wakurugenzi ya Klabu ya Arusha United ya jijini hapa, imetangaza kuiondoa timu hiyo kushiriki katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kile walichodai Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kushindwa kusimamia ligi hiyo ipasavyo.

 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Arusha United, Otte Beda, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, alisema kuna vitendo vinafanyika katika ligi hiyo ambavyo siyo vya kianamichezo.

 

Alidai kuwa vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinafanywa na viongozi wa timu zinazoshiriki ligi hiyo, hasa timu zinapocheza katika viwanja vya ugenini pia upangaji wa matokeo ambayo huwa inafanywa na waamuzi kwa kuwabeba wapinzani, ambapo wao waliiandikia barua kadhaa TFF juu ya malalamiko lakini wameona kimya.

 

“Bodi ya Arusha United ilikutana na kujadiliana na hatua gani TFF inachukua kuhakikisha kwamba mambo hayo hayaendelei, lakini baada ya kutafakari kwa kina na kuangalia historia ya ligi hii tukajiridhisha kuwa hakuna dalili zozote zinazoweza kuchukuliwa na TFF,” alisema.

 

Aliongeza kuwa baada ya bodi kuona hivyo, kama wataendelea kushiriki kwenye ligi ambayo vitendo vya kihuni vinaruhusiwa na kufumbiwa macho huku hakuna hata dalili zozote za lazima za hatua kuchukuliwa, watakuwa hawana utofauti na wahuni ambao wanashiriki ligi hiyo.

 

Alisema kuonyesha wanapinga vitendo hivyo na kutoa changamoto kwa TFF, kuhakikisha wanafanya mabadiliko ya usimamizi katika Ligi Daraja la Kwanza wameamua kujitoa kuanzia jana Machi 21, 2019.

 

Kwa hatua hiyo maana yake ni kuwa timu hiyo haitacheza mechi zake tano za Kundi B zilizosalia, mbili za ugenini na tatu za nyumbani.

 

Alisema kuna baadhi ya vitendo vya uvunjifu wa amani na hujuma ambazo timu ya Arusha United imefanyiwa katika baadhi ya mechi zake za ugenini na waliandika barua ya malalamiko TFF lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

 

Akitolea mfano aliutaja mchezo wa Rhino Rangers dhidi ya Arusha United wa Februari 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora. “Viongozi wetu walifanyiwa fujo na mashabiki wa Rhino na baadhi yao kupigwa, mchezo dhidi ya Dodoma FC wa Jamhuri mjini Dodoma, waandishi wetu walizuiwa kurekodi mechi licha ya kuwa na kibali cha TFF kinachoruhusu kurekodi mchezo huo,” alisema.

 

Aliendelea kutaja matukio kadhaa ya uvunjifu wa Amani yaliyotokea kati ya wao dhidi ya Transit Camp (Uwanja wa Azam Complex), dhidi ya Polisi Tanzania (Uwanja wa Ushirika).

 

Aliongeza kuwa watajadiliana kuhusu hatima ya wachezaji wao na mali za klabu kwa kuwa wanajua haki za wachezaji wao na hawatazivunja.

Comments are closed.