The House of Favourite Newspapers

AIBU! NJEMBA ANASWA WIZI NGUO ZA NDANI ZA KIKE

MBEYA: AMEJUA kutuweza! Kwa kawaida wizi haukubaliki na utakapotiwa mbaroni kwa wizi ujue yatakukuta makubwa, lakini utakapodakwa katika tukio la kuiba nguo za ndani, itakuwa ni aibu yako.

 

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa kijana Ulisubisya Kabuka (28) mkazi wa Forest ya zamani jijini hapa, ambaye amefanya tukio la aibu la kuiba nguo za ndani za kike.

 

Katika tukio hilo lililotokea Machi 27, mwaka huu, Kabuka alitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani hapa baada ya kukamatwa na vidhibiti vya nguo za ndani za kike za wakubwa mbili na za watoto kumi, ambazo zina thamani ya Tsh. 42,000.

 

Maelezo yaliyopatikana eneo la tukio yanasema kuwa, Kabuka alifika katika duka la mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina la Asia Minga (28), eneo la Mwanjelwa katika chumba namba 366 na kufanya tukio hilo la wizi.

 

“Alifika dukani majira ya saa 10 jioni, akiwa na mfuko wa mbolea, lakini akiwa hapo aliiba nguo za ndani na kuziweka kwenye mfuko wake wa mbolea. Bahati nzuri alishtukiwa, alivyoulizwa akatupa ule mfuko wa mbolea na kuanza kukimbia,” anasema Shadrack Mwakapijila aliyeshuhudia tukio hilo.

 

Shuhuda mwingine Hadja Bwera naye anasimulia: “Kelele za mwizi zilimshtua huyo jamaa, akaanza kukimbia kutoka juu (duka lipo ghorofani) na kuanza kushuka kwa kasi, askari mgambo walikuwa wameshamuona, wakamuwahi na kumdhibiti.”

 

Baada ya mgambo wa jiji kufanikiwa kumkamata, walimfikisha moja kwa moja katika Kituo cha Polisi Mwanyelwa ambapo Kabuka wakati akitoa maelezo yake, alisikika akisema: “Mimi siyo mwizi, mimi nilidhani hizo ni takataka, nashangaa huyu dada ananifukuza akidai nimemuibia.”

 

Kwa upande wake Asia alisema akiwa chumba cha jirani yake alimuona mtuhumiwa akiingia katika chumba chake na alipomuhoji alianza kutimua mbio ndipo alipopiga yowe na wafanyabiashara wakishirikiana na mgambo wa jiji wakafanikiwa kumkamata na kumpeleka polisi.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo aliwapongeza wafanyabiashara hao kumkamata mtuhumiwa bila kumdhuru kwani hiyo ndiyo dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi. Alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo, mtuhumiwa huyo atapandishwa mahakamani.

Comments are closed.