The House of Favourite Newspapers

IZZO B AMFUNGUKIA GODZILLA, PANCHO


RAPA kutoa Mbeya City, Emmanuel Simwinga ‘Izzo Bizness’ amemfungukia rapa mwenzake, marehemu Godzilla na Pancho Latino kuwa ni kati ya waliokuwa marafiki zake wa karibu mitandaoni.

Akifunguka mbele ya vipaza sauti vya +255 Global Radio kupitia Kipindi cha Bongo 255, Izzo Bizness anayetikisa kwa sasa na Ngoma ya Midadi aliyomshirikisha Aslay aliyasema hayo alipoulizwa juu ya kuwa na wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii na faida zake kama msanii.

“Ujue kwanza nasikitika akaunti yangu ya Instagram wajanja wameidukua ilikuwa na wafuasi zaidi ya milioni 1.5. Mitandao wakati mwingine inachangia fursa lakini siyo wote waliopo kwenye mitandao basi wanakuwa wapo ‘active’.

“Mfano katika akaunti yangu hiyo alikuwepo Godzilla, Pancho kwa sasa hawapo lakini bado ilikuwa ikisomeka hivyo, hapo hujajua kuna wengine waliibiwa simu zao na wengine hatunao kwa hiyo siamini kwa asilimia kubwa kama kuwa na wafuasi wengi basi unapata faida sana kama msanii,” alisema Izzo B na kuongeza;

“Redio na shoo bado zina nguvu kubwa kuliko mitandao kwa sasa wanaokusikiliza na kukuona kwenye shoo siyo wote wanaokufuatilia mitandaoni. Unaweza kwenda kwenye shoo ukashangaa kati ya 1,000 ni watano tu au kumi wana ‘smartphone’.”
Izzo B pia aliongelea ujio wake wa ngoma mpya ya Midadi kuwa ilimchukua mwaka na nusu kuiweka ndani hadi alipoiachia.

“Wakati mwingine ni mipango tu, nilitengeneza ngoma ya Midadi na Aslay mwaka na nusu uliopita nikaona kipindi hiki ndiyo cha kuachia. Lakini ukiachana na hilo pia nina ngoma nyingine nimemshirikisha Rayvanny amefanya Mr T Touch bado haijatoka japo nimeshamtumia Babu Tale na Diamond kwa hiyo tunasubiri taratibu zao kama lebo si unajua kila sehemu ina utaratibu wake,” alimaliza kusema Izzo B.

Je, umeshasikiliza redio janja ya +255 Global Radiokupitia simu yako ya mkononi? Kama bado ni rahisi  sana, ingia katika Playstore kwenye simu yako ya kiganjani kisha download APP ya 255 Global Radio na usikilize vipindi vyote vya kijanja mjini.
Imeandaliwa: Andrew Carlos/GPL

Comments are closed.