The House of Favourite Newspapers

Bil 20 Zamng’oa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi

SPOTI Xtra limejiridhisha kwamba kilichomng’oa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi kwenye uongozi ni Sh.Bil 20 za uwekezaji. Simba ilitangaza jana kwamba, Mkwabi ameachia ngazi na taratibu za kuziba nafasi yake zitawekwa wazi hivi karibuni.

 

Habari za ndani zinasema kwamba, kumekuwa na mzozo ndani ya uongozi kuhusiana fedha hizo zilizopaswa kuwekezwa na bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ jambo ambalo lilimsukuma Mkwabi kuandika
barua ya kujiuzulu na kuikabidhi kwa bodi wiki kadhaa zilizopita kabla haijatangazwa jana.

 

Mo aliahidi atatoa mabilioni hayo baada ya makubaliano ya mfumo mpya wa mabadiliko ya kuwa kampuni mara baada ya kupatiwa asilimia 49 huku 51 ya hisa ikibakia kwa wanachama.

 

Uchunguzi wa Spoti Xtra umebaini kwamba, kiasi hicho cha fedha hadi sasa bado hakijaingizwa ndani ya klabu hiyo ambayo wanachama ndiyo wanawakilishwa na Mkwabi kwenye Bodi.

 

Habari zinasema kwamba, licha ya hatua za awali kufanyika lakini bado mchakato umekuwa mgumu kutokana na Mo kuhitaji uhakiki wa thamani za Simba ikiwemo majengo na ardhi huku baadhi ya wanachama wakiweka ngumu kutoa nyaraka za umiliki wa jengo kwa kwa madai kuwa mali hizo ni za wanachama siyo za kampuni.

 

Mo alifanikiwa kupata nafasi ya kuwa mwekezaji ndani ya klabu ya Simba baada ya kuyashinda baadhi ya makampuni yaliyojitokeza kufanya uwekezaji ndani ya klabu hiyo mwaka jana na kuahidi kutoa kiasi cha Sh.Bil 20.

 

Simba iliingia katika mfumo mpya wa mabadiliko ya klabu kwa kufanya uchaguzi mkuu Novemba 4, mwaka jana ambao ndio ulimuweka Mkwabi madarakani na kuwa sehemu ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo chini ya mwekezaji Mo Dewji ikiwa na wajumbe 16 nane kutoka upande wa mwekezaji nane upande wa wanachama.

 

Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata kutoka Simba zinasema kuwa, Mkwabi aliandika barua ya kuachia ngazi wiki kadhaa zilizopita kwa madai kwamba hataki kuingia kwenye lawama za wanachama ambao ndio waliomchagua.

“Mkwabi ameamua kuachia ngazi ndani ya Simba kutokea kutoelewana ndani ya bodi kila anapohoji ishu ya Sh.Bil 20, ndio maana amechukua uamuzi huo ili kuepuka mgogoro zaidi ambao unaweza kujitokeza kwavile hata wanachama wanamshinikiza sana kwavile wengi wao wanaona muda unakwenda tu na hawaelewi,” kilisema
chanzo chetu na kuongeza: “Lakini kingine anaona kama mambo yanapokwenda anaweza kuja kuonekana mbaya kwavile yeye kasimama katikati ya kampuni na wanachama, na pengine inaweza kumuingiza kwenye matatizo binafsi ambayo yanaweza yakaathiri mpaka maisha yake mengine ndio maana kaamua kuandika barua.

 

“Hiyo barua ipo kwenye bodi hata kabla ya Simba Day, ila walimwambia akaushe kwanza,” kiliongeza chanzo chetu cha uhakika. Baada ya Simba kutoa taarifa jana, Spoti Xtra lilimtafuta Mkwabi lakini hakutaka kuzungumza chochote zaidi ya kusisitiza kwamba atazungumza wakati ukifika.

Comments are closed.