The House of Favourite Newspapers

Shinyanga: Madereva Bodaboda 57 Wanyakuliwa

MADEREVA pikipiki maarufu kama bodaboda 57 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Shinyanga baada ya kubainika kukiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kupakia abiria zaidi ya mmoja na wengine kutokuwa na kofia ngumu.

 

Ukamataji huo imefanyika wilayani Kahama na kuongozwa na Mkuu wa kitengo cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga, Anthony Ng’wandu na kusema kuwa Oparesheni Nyakuanyakua tayari imeshaanza kutekelezwa kwa mkoa mzima na kwa dereva yeyote atakayekiuka sheria za usalama barabarani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

 

Amesema jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa madereva bodaboda wazembe ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani huku baadhi ya madereva waliokamatwa katika oparesheni wiyo wakiwaomba madereva wenzao wazingatie sheria hizo.

 

Amefafanua kuwa miongoni mwa makosa ambayo wamekamatwa waendesha bodaboda hao ni pamoja na kuzidisha abiria, kutokuwa na kofia ngumu, kutozingatia matumizi ya alama za barabarani kama vile taa na vivuko vya watembea kwa miguu.

 

Paschal Mihayo na Fundikira Saidi ni miongoni mwa madereva waliokamatwa katika oparesheni hiyo  ambapo wamekiri kukiuka sheria za usalama barabarani na kuwataka madereva wenzao kuhakikisha wanatii sheria bila shuruti.

 

Wameliomba polisi kuendelea kutoa elimu kwao ili kuhakikisha sheria hizo zinaheshimiwa kwa kuzuia ajali ambazo zimekuwa zikitokea.

Comments are closed.