The House of Favourite Newspapers

Simba, Yanga Ubingwa Upo Hapa!

0

HIVI sasa Simba inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 53, huku Yanga ikiwa ni ya tatu na pointi zake 38.
Simba ikiwa imecheza mechi 21 na Yanga 19, zinatarajiwa kupambana Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo unatajwa kwamba ndiyo utaamua bingwa wa ligi msimu huu.

Kama ilivyokuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, ndiyo ilivyo mchezo huu kwani awali ilionekana atakayeshinda ndiye ana nafasi kubwa ya kuwa bingwa, lakini mwisho wa siku matokeo yakawa 2-2.

Kuelekea mchezo huu wa mzunguko wa pili, Yanga inatarajiwa kucheza mechi tano kabla ya kukutana na Simba. Safari hii Yanga watakuwa wenyeji wa mchezo huo.


Kwa upande wa Simba, nao watacheza mechi tano kabla ya kukutana na Yanga. Mechi hizo zinatajwa kuwa zinaweza kuwa kikwazo kwa wote katika kuelekea kutwaa ubingwa msimu huu.

Jumamosi ya wiki hii, timu hizo zote zitakuwa uwanjani, Yanga itacheza dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, wakati Simba ikipambana na Lipuli kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Mechi tano zijazo za Yanga, tatu itachezea nyumbani dhidi ya Prisons, Alliance na Mbao, huku za ugenini ni dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal.

Yanga ilipokutana na timu hizo katika mzunguko wa kwanza, iliambulia pointi kumi baada ya kushinda tatu na sare moja, huku ikiwa bado haijacheza na Mbao. Matokeo yalikuwa hivi; Prisons 0-1 Yanga, Yanga 3-3 Polisi TZ, Yanga 1-0 Coastal na Alliance 1-2 Yanga.

Kwa Simba, yenyewe itacheza mechi moja tu nje ya Dar dhidi ya Lipuli, kisha baada ya hapo, zinazofuata ni jijini Dar dhidi ya Kagera Sugar, Biashara United, KMC na Azam.

Simba ilipocheza dhidi ya timu hizo katika mzunguko wa kwanza, matokeo yalikuwa hivi; Simba 4-0 Lipuli, Kagera 0-3 Simba, Biashara 0-2 Simba, KMC 0-2 Simba na Simba 1-0 Azam ambapo ilikusanya pointi 15 kwa kushinda zote.
Endapo hali itakuwa hivyo hadi wanakutana, ni wazi Simba itakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu kwani hivi sasa imeiacha Yanga kwa pointi 15.

Leave A Reply