The House of Favourite Newspapers

Video: Mkurugenzi Kilosa Aomba Radhi Mara tatu Rais Magufuli

0

ASAJILE Mwambambale, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro (DED), amemuomba radhi mara tatu, Rais John Magufuli, kwa kosa la kutotatua changamoto ya mgogoro wa ardhi wilayani humo.

 

Mwambambale amelazimika kuomba msamaha huo, baada ya kuandamwa na malalamiko ya kutowajibika katika utatuzi wa migogoro, yaliyoibuliwa na wananchi wa wilaya hiyo, leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020, katika ziara ya Rais Magufuli.

Mkurugenzi huyo wa Kilosa alikuwa anatuhumiwa kutosikiliza kero za wananchi kuhusu migogoro ya ardhi, pamoja na kuandika barua iliyokuwa inawakataza wananchi kutotumia mashamba yaliyokuwa yaliyokuwa yameuzwa kinyume cha sheria.


Kufuatia malalamiko hayo, Mwambambale amemuomba radhi Rais Magufuli huku akimuahidi atajirekebisha kwani amekwisha kytambua amejikwaa

 

“Rais ninaomba unisamehe, mheshimiwa rais ninaomba unisamehe, mheshimiwa rais ninaomba unisamehe,” amesema Mwambambale alipopewa fursa ya kuzungumza mbele ya Rais Magufuli na umati ya wananchi.

 

“Kuna kazi nyingine umenipa na nimefanya kwa mafanikio, kuna miradi ya maendeleo mbalimbali nimejenga. Najifunza naomba unisiamehe, naomba unipe nafasi ya pili sitokuangusha,” amesema Mwambambale kwa sauti ya unyonge

Kabla ya Mwambambale kuomba toba hiyo, Rais Magufuli alimuuliza Seleman Jaffo, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, historia ya utendaji kazi wa mkurugenzi huyo, ambaye alikiri utendaji wake kuwa na dosari, kutokana na malalamiko mengi ya wananchi wa wilaya yake.

 

“Rais kutoa haki kuna kazi nzito sana, kwa haraka, kwa taarifa ambazo juzi nimepata kutoka kwa mkuuu wa mkoa, kuna eneo liliuzwa hapa. Na mheshimiwa Rais nilikujulisha kuhusu hili eneo na hili ulilitolea maelekezo kule tulikotoka,” amesema Jaffo na kuongeza:

 

“Kila mwananchi analalamika kwa upana wake, nadhani ungelitathimini kwa upana jambo hili. Lakini ni fundisho kwa viongozi wengine, kwa nini wananchi wote wanalalamika? Hili halina afya kabisa kwa nyinyi mliokuwa na dhamana hili jambo sio sawa, malalamiko hayatoi taswira nzuri,” amesema

Baada ya Jaffo kutoa kauli hiyo, Rais Magufuli alimpa onyo mkurugenzi huyo na kumtaka kuandika hadharani barua ya kutengua maamuzi yake ya kuuza mashamba hayo pamoja na kuwaomba radhi wananchi kwa dosari zilizojitokeza.

“Mkurugenzi hiyo barua uliiandika wewe, andika chini ya barua hii (barua hiyo ya zuio) useme nimefuta mwenyewe na ninaomba msamaha kwa wananchi, kama huwezi kuandika niende na barua zangu nikaamue mimi mwenyewe nitakavyoamua kuandika,” amesema Rais Magufuli.

 

Mkurugenzi huyo alikubali na kuandika kisha kuirejesha kwa Rais Magufuli ambaye alisema kwa kuwa ameomba msamaha, anasamehewa na kumtaka kujirekebisha.

Leave A Reply