The House of Favourite Newspapers

Mkenya Ampisha Kiungo Matata Yanga SC

0

UPO uwezekano mkubwa wa Klabu ya Yanga kuachana na kipa wake, Faroukh Shikhalo raia wa Kenya kwenye usajili wa dirisha dogo ili ampishe kiungo mchezeshaji wa kimataifa katika kukiimarisha kikosi hicho.

 

Dirisha la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu huku timu hiyo ikiwa tayari imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji, Mrundi, Said Ntibazonkiza ‘Saido’.

 

Yanga imepanga kufanya usajili wa wachezaji watatu kati ya hao wapo wazawa na kimataifa waliokuwepo kwenye mazungumzo ya mwisho na timu hiyo na kiungo anayetajwa kutua Yanga ni Isah Ndala anayekipiga Plateau United ya nchini Nigeria.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Yanga imepanga kuachana na Shikalo ili wapate nafasi ya mchezaji wa kigeni atakayejiunga na timu hiyo.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Yanga itaachana na kipa huyo baada ya kushindwa kuonyesha ushindani mbele ya kipa namba moja wa timu hiyo, Metacha Mnata aliyekuwepo kwenye kikosi cha Taifa Stars.

 

Aliongeza kuwa, wakijiandaa kuachana na Shikhalo, upo uwezekano mkubwa wa timuhiyo kumsajili kipa mwingine atakayempa changamoto Metacha na Ramadhani Kabwili.“

 

Yanga imepanga kufanya mabadiliko kidogo ya usajili katika dirisha dogo na wamepanga kusajili wachezaji watatu pekee kati ya hao wapo viungo na mabeki watakaojiunga na timu katika msimu huu.

 

“Hiyo ni baada ya kocha kufanya mapendekezo ya usajili wa wachezaji wapya na wale watakaowatoa kwa mkopo na kuachana nao jumla baada ya kushindwa kuonyesha ushindani katika timu.“

 

Kati ya wachezaji ambao huenda wakaachwa ni Shikalo ambaye yeye amekosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na kujikuta akikalishwa benchi na Metacha.“

 

Hivyo mabosi wake huenda wakaachana naye ili wapate nafasi ya usajili ya mchezaji wa kimataifa, Shikalo ni kipa mzuri lakini ameshindwa kumpa upinzani Metacha,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano wa Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alisema kuwa: “Jukumu la usajili lote lipo chini ya Kocha Kaze (Cedric) ambaye atatoa mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji na atakaowaacha.”

 

Kwa upande wa Kaze yeye alisema kwa hivi sasa akili yake ameielekeza katika kumalizia michezo waliyoibakisha ya Ligi Kuu Bara kwa lengo la kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni.

Wilbert Molandi,Dares Salaam

Leave A Reply