The House of Favourite Newspapers

Nabi Mafia, Kaharibu Mipambo ya Gomez

0

KOCHA Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba, anatarajiwa kupangua kikosi chake, huku lengo kubwa likiwa ni kupata ushindi.

 

Hiyo ni katika kuelekea Kariakoo Dabi itakayowakutanisha watani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga itakayopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Kitendo cha Nabi kupangua kikosi, itakuwa ni sehemu ya kutegua mitego ya Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, aliyewaomba mabosi wake video za michezo miwili ya Yanga dhidi ya Zanaco na Rivers United ili asome mbinu zao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar, upo uwezekano mkubwa wa kikosi cha Nabi kikawa na mabadiliko kadhaa.

Mtoa taarifa huyo aliwataja wachezaji wanne watakaoingia katika kikosi chake ni Shaban Djuma, Fiston Mayele, David Bryson na Khalid Aucho atakayechukua nafasi ya Mkongomani, Mukoko Tonombe anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata msimu uliopita.

Alisema kuwa katika mchezo huo, Aucho atacheza kiungo mkabaji namba sita na Zawadi Mauya atasogezwa mbele kucheza nane badala ya sita nafasi anayoicheza tangu ajiunge na Yanga.

“Jana (Jumanne) jioni tulicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya DTB inayoshiriki Championship ambayo tuliifunga mabao 3-1, katika mchezo huo Kocha Nabi alionekana kuwaingiza kikosini wachezaji wake wanne waliokosekana katika michezo yetu dhidi ya Rivers.

 

“Kocha aliomba mchezo huo wa kirafiki kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake kabla ya kukutana na Simba, aliwaingiza wachezaji hao wanne kwa lengo la kutengeneza muunganiko wa timu.

 

“Wachezaji hao ni Mayele, Bryson, Aucho na Djuma ambao walikosekana katika michezo ya kimataifa, huenda Aucho akacheza namba sita iliyokuwa inachezwa na Mauya ambaye atapangwa nane nafasi inayochezwa na Tonombe ambaye atakosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema: “Maandalizi yanaendelea vizuri kambini kwetu Avic Town na wachezaji wapo katika morali ya juu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

“Kikubwa salamu ziwafikie watani kuwa, wachezaji wetu wote waliokosekana katika michuano ya kimataifa ambao ni Aucho, Mayele, Djuma na Bryson watakuwepo.”

Leave A Reply