The House of Favourite Newspapers

Mbosso: Kupata Mwanamke wa Kuoa ni Kazi Sana “Nitatamani Kumrudisha Marehemu Martha”

0

 

 

 

UKIMTOA Marioo na utunzi wake mzuri wa mashairi ya mapenzi, kuna mwamba mwingine anatikisa vilivyo kwenye sekta hiyo. Huyu si mwingine, namzungumzia Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso Khan. Mashabiki wa ngoma zake na waliomshuhudia akipafomu ‘live’ stejini watasadiki maneno yangu kuwa huyu jamaa ni noma.

 

Mbosso amefanya ngoma nyingi na kali mno. Miongoni mwake ni Mtaalam, For Your Love, Yalah, Nadekezwa, Tamba, Hodari, Baikoko, Tamu, Haijakaa Saw, Fall na nyingine kibao.

 

Tangu mwaka 2022 uanze, IJUMAA SHOWBIZ haijakaa na Mbosso kwenye ‘one on one’, lakini sasa huyu hapa wakati huu akitamba na ngoma ya Oka aliyoshirikishwa na Diamond Platnumz ambapo amefunguka mambo mengi kuhusu maisha yake ya kazi na maisha kwa jumla.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi?

MBOSSO: Poapoa karibu.

IJUMAA SHOWBIZ: Asante, hivi mpangilio wa ratiba yako asubuhi huwa ukoje?

MBOSSO: Mimi huwa naamka saa 11:00 au saa 12:00 asubuhi, nakwenda kucheza mpira kisha narudi nyumbani kwa ajili ya kupata chai.

IJUMAA SHOWBIZ: Nilitegemea utaniambia huo muda unaoamka huwa unafanya mazoezi kidogo kama ilivyo kwa baadhi ya mastaa wengine, vipi hupendi au ni uvivu tu?

 

MBOSSO: Sina muda mrefu sana tangu nianze kwenda

kufanya mazoezi, kwa hiyo ikitokea siku nimeamka asubuhi kisha sijaenda uwanjani kucheza mpira basi huwa naenda gym.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Wanasema wanaume ambao hawapendelei kunywa pombe, basi starehe yao kubwa huwa ni wanawake, vipi kwa upande wako?

 

MBOSSO: (anacheka) sio kweli bwana! Mbali na muziki pamoja na kucheza mpira wa miguu, starehe yangu nyingine napenda kucheza Play Station (PS), kuangalia muvi na kupiga gitaa.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Sasa ikawaje umezaa na wanawake wengi kiasi hicho na bado umri wako ni mdogo?

MBOSSO: Watoto ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, sasa unakuta kuna muda mwanamke ambaye umezaa naye amezingua au mmezinguana na hamuwezi kuendelea kuwa pamoja ndiyo unajikuta umeangukia sehemu nyingine.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Inasemekana kwamba huwa hupendi kupokea namba ngeni ya simu, je, ni kweli?

 

MBOSSO: Ni kweli sipokei namba ngeni kwa sababu huwa napigiwa na namba mpya nyingi sana.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Imeshawahi kukutokea hujapokea namba ngeni, halafu kumbe ilikuwa ni ya muhimu?

 

MBOSSO: Mara nyingi sana imeshanitokea, lakini badala yake huwa wanajua namna gani ya kunipata.

IJUMAA: Umesema unapenda sana mpira wa miguu, tuambie unashabikia timu gani?

MBOSSO: Kwa ndani nashabikia Simba na kwa nje napenda Chelsea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mchezaji gani ambaye anakuvutia?

MBOSSO: Kiukweli bila kupepesa macho nampenda sana Christiano Ronaldo japokuwa hachezei Chelsea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Binadamu yeyote anapokumbwa na msongo wa mawazo huwa na njia ya kufanya ili kuondoa mawazo yake, hii imekaaje kwa upande wako?

 

MBOSSO: Mara nyingi nikiwa na mawazo napenda sana kuangalia muvi za Kihindi na kusikiliza muziki.

IJUMAA SHOWBIZ: Upo kwenye uhusiano wa kimapenzi?

MBOSSO: Ndiyo, nina mpenzi

 

IJUMAA: Na mmoja kati ya mama watoto wako au mpenzi mpya?

MBOSSO: (anacheka) wewe jua tu nipo kwenye uhusiano na nampenda sana mpenzi wangu.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Jambo gani ambalo umewahi kulipoteza huko nyuma ukipewa nafasi leo hii utatamani kulirudisha?

MBOSSO: Nitatamani kumrudisha marehemu Boss Martha (mzazi mwenzake) kwa sababu ni mwanamke ambaye bado namkumbuka na nashindwa kabisa kumsahau.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Unamuenzi vipi?

MBOSSO: Kila ikifika tarehe 11 ya kila mwezi huwa naenda kwenye kaburi lake kutembea na kuzungumza naye, huwa namwambia vitu vingi sana ikiwemo kumwelezea kila kinachoendelea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Umesema kwamba upo kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine na bado unasema umeshindwa kabisa kumsahau marehemu Martha, hii huwa haimpi wakati mgumu mpenzi uliyenaye kwa sasa?

 

MBOSSO: Kitu kingine ambacho watu hawakijui ni kwamba unaweza ‘uka-move on’ na ukajiona upo kwenye uhusiano, lakini usiwe na uhakika, asikuambie mtu inaboa sana, yaani kwa mtu ambaye ananipenda sasa hivi namboa hadi yeye mwenyewe anajua kuwa namboa na hii yote ni kwa sababu bado sijamsahau kabisa marehemu.

IJUMAA SHOWBIZ: Kitu gani kikubwa ambacho unakikumbuka kutoka kwake?

 

MBOSSO: Nakumbuka mambo mengi sana kutoka kwake, ‘beautiful moments’ ambazo tulikuwa tunapata nafasi ya kukaa pamoja, mipango tuliyokuwa nayo na vingine vingi.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Jambo gani la mwisho ambalo uliongea naye kabla ya umauti kumfika?

 

MBOSSO: Nakumbuka kabla hajafariki dunia, tulikuwa tunatafuta nyumba kubwa kwa ajili ya yeye kukaa na mtoto, lakini kwa bahati mbaya kifo kikamchukua.

IJUMAA SHOWBIZ: Pole sana.

MBOSSO: Nashukuru sana.

IJUMAA SHOWBIZ: Jambo gani ambalo umewahi kulifanya kwa hasira halafu baadaye ukajutia kwa nini umelifanya?

MBOSSO: Mimi nina hasira sana na mwepesi wa kupaniki, kwa hiyo kuna muda huwa inatokea nakasirika na kutoa kauli mbaya, lakini baadaye huwa najirudi na kuona kitu nilichokiongea siyo kizuri.

IJUMAA SHOWBIZ: Unatamani kuoa mwanamke mwenye vigezo gani?

MBOSSO: Mwanamke ambaye nikiingia nyumbani kwangu afahamu kwamba nimerudi nyumbani na ajue kwamba nimerudi kama mumewe na siyo msanii, lakini pia nikiwa natoka ajue kwamba naenda kazini kama msanii, wapo wachache, kupata mwanamke wa kuoa ni kazi sana.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamzungumziaje Zuchu kwa sasa?

MBOSSO: Ile imani tuliyokuwa nayo kwake wakati anatambulishwa WCB hatimaye amezidi kuiongezea thamani, namaanisha kitu tulichokuwa tunataka kukiona kwake ndicho ambacho tunakiona kwa sasa, tangu ameanza, hajawahi kuuangusha uongozi mzima wa WCB anafanya kazi nzuri sana tena kwa kujituma hivyo namuona mbali kisanaa.

IJUMAA SHOWBIZ: Umeshawahi kwenda kwa mganga?

MBOSSO: (anacheka), hapana sijawahi kwa kweli.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamuongelea vipi Diamond?

MBOSSO: He is my role model, ni bosi wangu, amemtoa Marombosso amemleta Mbosso Khan.

Leave A Reply