The House of Favourite Newspapers

Smith Afungiwa Kushiriki Tuzo za Oscar kwa Miaka 10, Aachiwa Tuzo Aliyoshinda

0
                       Will Smith amefungiwa kwa kipindi cha miaka 10 kushiriki tuzo za Oscar

MWIGIZAJI maarufu Duniani kutoka nchini Marekani Will Smith amefungiwa kwa kipindi cha muda wa miaka 10 kujihusisha na Tuzo za Oscar baada ya kumpiga kofi mchekeshaji Chris Rock katika tuzo za Oscar zilizotolewa mwishoni mwa mwezi Machi.

 

Pamoja na adhabu hiyo Will Smith ameruhusiwa kuendelea kumiliki tuzo aliyopokea katika sherehe za utoaji tuzo za Oscar ya muigizaji bora wa mwaka.

 

Katika taarifa iliyotolewa na Uongozi wa Tuzo za Oscar imesema:

 

“Wakati shughuli inaendelea kuoneshwa mubashara hatukuweza kuliongelea na kulikemea tukio  kwa hilo tunaomba mtusamehe sana, Bodi imeamua kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia Aprili 8, 2022 Will Smith hataruhusiwa kuhudhuria tukio lolote lile linalohusiana na Tuzo za Oscar iwe yeye mwenyewe au kwa kumuagiza mtu lakini pia tunamshukuru Rock kwa kuwa mvumilivu na muelewa hasa katika kipindi kigumu kama kile na kwa namna ya pekee tunawashukuru wageni, waendesha vipindi, washiriki na washindi wote wa zawadi siku ile kwa utulivu wao wakati wote wa matangazo ya moja kwa moja.”

           Will Smith akimchapa kibao Chris Rock katika sherehe ya Tuzo za Oscar mwishoni mwa mwezi Machi

Mara baada ya maamuzi hayo kutolewa, Will Smith kupitia jarida la Deadline alisema:

 

“Nakubali na naheshimu maamuzi ya Bodi ya Tuzo za Oscar.”

 

Zaidi ya wanachama 9,000 walikasirishwa na kitendo kile na kusisitiza Will Smith anyang’anywe tuzo aliyopokea.

 

Mke wa Will Smith, Jade Will yeye ameruhusiwa kuendelea kuhudhuria tuzo hizo, mara baada ya tukio hilo Jade alihojiwa juu ya tukio lilifanywa na mme wake na alidai kwamba angetamani mume wake asingefanya tukio lile.

 

Tangu kutokea kwa tukio la kupigwa kibao kwenye steji mchekeshaji Chris Rock hajatamka neno lolote la kuashiria kuchukua hatua badala yake amekuwa ni mtu aliye kimya na mara kadhaa anapohojiwa amekuwa akisema kuwa bado analifanyia kazi suala hilo.

Leave A Reply