The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani-24

0

ILIPOISHIA: “Ooh! Murembo mutoto muzuri!” “Ndiye mimi,” nami nilijishebedua. “Uko sawa?” “Ndiyo.” “Sasa sikiliza, samahani leo hatutaonana nina safiri ya ghafla  nakwenda Marekani usiku huu, nitarudi baada ya wiki kwa hiyo sitaki ufanye biashara ya mwili sawa?” SASA ENDELEA…

“ Nisifanye vipi ikiwa hiyo wiki hutakuwepo nitakula nini?” “Mwasiiii Kitokooo, leo nimekupa bei gani, tangu ulipoanza kufanya hiyo biashara ulishawahi kupata pesa nyingi kiasi hicho? Hiyo pesa hata nikikaa miezi mitatu huwezi kuimaliza.”

“Si ulinipa kwa kazi ya jana?” “Tuliongea nini, nimekueleza nataka kubadili maisha yako mbona unakuwa si muelewa?” “Sawa basi nimekuelewa, nitakusubiri.” “Vizuri, leo atakuja yule kijana usiku huu atakuletea pesa na nguo ambazo unatakiwa kuzivaa, sawa?” “Sawa.” “Wewe hupendi kuendesha gari la kifahari?” “Napenda.” “Hutaki kumiliki jumba kama langu?” “Nataka.”

“Hutaki kuwa na mwanaume mwenye pesa kama mimi?” “Nataka.” “Basi nikirudi tutafanya kazi moja matata itakayobadili maisha yako.” “Sawa Papaa.” “Na kama unataka kujirusha akija dereva wangu mwambie akupeleke ukumbi wowote unaotaka kwa gharama yangu na kukurudisha.” “Sawa Papaa.” “Nakupenda sana murembo.”

“Hata mimi Papaa nakupenda sana.” “Basi nikuache upumzike.” “Asante na wewe nikutakie safari njema mpenzi wangu uende salama urudi salama.” ‘Asante, nikuletee zawadi gani mpenzi wangu?” “Yoyote mpenzi wangu.” “Hakuna tatizo.”

Baada ya mazungumzo na Papaa nilikata simu na kumgeukia Doi aliyekuwa akifuatilia mazungumzo yetu kwa muda mrefu. “Mmh! Makubwa,” nilisema kwa sauti. “Makubwa hasa, kuna biashara kweli hapo naona mapenzi yametawala, vipi kuna mtoko kweli maana nasikia safari njema, aende salama arudi salama kulikoni?” “Mmh! We acha tu, mzee kapata safari ya ghafla.” “Anakwenda wapi?” “Marekani.” “Acha! Kufanya nini?”

“Anajua mwenyewe.” “Sasa mlikuwa mnabishana nini?” Nilimweleza Doi tulichokuwa tunabishana, shoga yangu alinilaumu na kuniambia: “Shoga zigo la pesa unataka kulipiga teke, kwa nini unamshika mkono kipofu wakati wa kula? Hatupendi kupigwa na baridi na kuliwa na mbu kila siku, sote tunatafuta unafuu wa maisha, unaangalia biashara yenu kama inalipa kula maisha kama hailipi achana nayo rudi tuendelee na harakati zetu.”

“Nisamehe shoga nilijisahau,” nilitambua nimefanya kosa. “Wewe fanya anavyotaka kisha tuone mwisho wake.” “Mmh! Sawa, kwa hiyo tutatoka?” “Lazima tutoke tukale raha kuna mtu anakuja muda si mrefu kutufuata.” Majira ya saa tatu usiku mtu aliyetumwa na Papaa alikuja kuniletea mzigo aliotumwa kuniletea, kwa vile nilielezwa nimweleze ninachokikata.

Nilimwambia atupeleke kwenye moja ya night club kwenda kujirusha, alitupeleka  na kutusimamia mpaka tunarudi. Siku ile yule kijana nilimpa ofa ya kwenda kulala na Doi bila malipo kwa vile pesa niliyokuwa nayo ningeweza kumpa shoga yangu.

*** Baada ya wiki Papaa alirudi na kutuma ujumbe siku ile tukutane kwake usiku, jioni ya siku ile nilivaa vizuri vitenge kama mwanamke wa Kikongomani kwa vile Papaa alikuwa Mkongomani basi alipenda kuona nikivaa vile. Kwa kweli nilipendeza sana na kuonekana mwanamke wa haja anayetakiwa kuolewa na kutulia ndani ya nyumba huku akilea watoto aliojaliwa na Mungu.

Hata dereva alinipotea kwa jinsi nilivyopendeza, sifa za kupendeza kwangu hazikuanzia kwa dereva tu, zilianzia kwa mashoga zangu kila mtu alimwaga sifa awezavyo. “Hakika Konso wewe ni mwanamke mzuri sana,” alisema Bahati. “Asante.”

“Konso nakuona kiumbe mwingine kabisa, nakuombea ukienda huko usirudi kwenye kazi yetu ya kupigwa baridi na kuumwa na mbu,” Doi naye aliongezea. “Asante jamani, niombeeni wito huu uwe wa heri ili tuvune wote naamini kama ni mafanikio yangu basi yamepitia mikononi mwenu.”


Nilisema kwa moyo wa uchungu mkubwa baada ya kuona jinsi gani tunaifanya kazi ya kuuza mwili kwa shingo upande huku nasi tukitamani maisha ya kumilikiwa na mtu au kufanya kazi zingine zisizo dhalilisha utu wa mwanamke. Usikose mwendelezo wake katika gazeti la risasi jumamosi.

Leave A Reply