The House of Favourite Newspapers

Video: A-Z Kutekwa Na Kukombolewa Kwa Madereva Congo

madereva-tekwa-12-001

Kikosi cha madereva waliotekwa nchini Congo.

Siku ya terehe 14 Septemba 2016 tukio la kutekwa kwa madereva wa Tanzania na waasi wa Maimai nchini Congo liligonga vichwa vingi vya habari duniani.

Madereva kumi walitekwa na kati yao wawili walifanikiwa kutoroka na kubaki nane. Madereva hao ni Kumbuka Selemani, Hussein Mohammed, Bakari Nassoro, Issa Omary, Amdani Zarafi, Adam James, Mbwana Said, Ali Juma, Athuman Fadhil na Amis Mshana.

Swali kubwa lilikuwa je? Baada ya madereva hao kutekwa na magari yao kuchomwa moto na waasi hao nini hatma yao? Macho na masikio ya watu wengi yalikuwa yakisubiri kusikia nini serikali ya Tanzania au Congo watasema kuhusiana na tukio hilo lililoleta sintofahamu kubwa kwa wananchi.

JINSI WALIVYOTEKWA

Mmoja wa madereva hao Kumbuka Selemani amesema tukio hilo lilikuwa kama sinema ya kuigiza:

“Siku ya tukio tulishusha saruji sehemu inaitwa Namoya jimbo la Kivu. Sasa wakati tunarejea tulikuwa kwenye msafara wa magari kama nane, mimi nikiendesha gari la nane.

“Ghafla tukasimamishwa na mtu aliyekuwa amebeba silaha nzito huku amevaa mavazi ya jeshi yasiyoeleweka, kwa maana ya kuchanganywa na kunitaka nishuke kwenye gari hilo na nimkabidhi kila kitu, ikiwemo hati yangu ya kusafiria na kadi ya gari.

“Wakati nimeshashuka niko chini namkabidhi vitu vyangu, mara lilitokea gari la tisa ambalo baada ya kumuona yule mwanajeshi, lilisimama na kuanza kugeuza kwa maana ya kukimbia. Ndipo yule askari akaachana na mimi akaanza kulirushia risasi lile gari lililokuwa linaendelea kugeuza.

“Mimi nilipoona ameelekeza mawazo yake kwenye yale magari nikapata upenyo na kukimbilia porini.

“Baada ya kutembea umbali mrefu porini nilikiona kikosi kingine cha polisi na baada ya kukichunguza nilibaini ni askari halali. Na baada ya kuwasogelea huku nimenyoosha mikono juu walinichukua na kunihoji na kunipa huduma ya kwanza.” Alisisitiza dereva huyo ambaye yeye alikuwa miongoni wa wale wawili waliofanikiwa kutoroka.

WALIOTEKWA

Dereva Athuman Fadhili yeye alikuwa kwenye kundi la watu nane waliotekwa na baadaye kukombolewa anasimulia.

“Nliliamriwa nishuke kwenye gari na kuwapa simu na passport kisha tukakusanywa wote na kuanza safari kuelekea mahali tusikokujua.

“Tulisafiri kama kilometa 30 zaidi kwenye msitu mnene. katika safari hiyo ya mateso ya siku mbili tulitembea usiku na mchana huku tukichanwachanwa na miba, tulifika kwenye eneo la kijiji ambacho hata hivyo kilikuwa na nyumba chache, tukaamriwa tutembee kwa kutambaa ili tusionekane na wanakijiji hao.

Baada ya kama kilometa tano kutoka kwenye hicho kijiji tulifika kwenye makazi ya muda ya watekaji hao na kukutana na mkubwa wao aliyejitambulisha kama Shehe Hassan aliyeamuru tupewe maji na kuanza kutuhoji majina yetu kupitia hati za kusafiria na kutaka kujua kuhusu familia zetu.

“Tuliteswa kwa kubebeshwa mizigo ya waasi tukiwa katika eneo hilo, mmoja wa viongozi wa watekaji hao aliyekuwa akizungumza kwa simu na bosi wao mwingine alitoa taarifa kuwa majeshi ya DRC yanawafuatilia hivyo wanatakiwa kujihadhari.

“Baada ya mahojiano hayo walipewa chakula na maji na kisha giza lilipoingia walitafutiwa eneo la kulala ambalo ni hema lililowekewa turubai. Majira ya saa sita au saa saba usiku huku mvua kubwa ikiwa inanyesha, tuliamshwa na kutakiwa kuendelea na safari kwa kuwa hali ya usalama katika eneo hilo ni tata kutokana na majeshi ya DRC kuzidi kuwakaribia.

“Tulikuwa tumechoka sana kutokana na kubeba mizigo yetu na yao safari nzima lakini tulilazimika kutembea tu. Ilifikia mahali tulitamani kupigwa hata risasi ili tupumzike na kuondokana na mateso tuliyokuwa tunayapata.

“Walitaka dola 4,000 kutoka kwa Dewji wakati wakiendelea kutembea, viongozi wa watekaji hao waliendelea kuwasiliana njia nzima na bosi wa Simba Logistics, Azim Dewji na kumpa saa 24 awe ametoa dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waachiwe huru.

“Lakini baadaye wao wenyewe wakaanza kubishana juu ya namna ya kuzipata fedha hizo kutokana na hali halisi ya msitu huo. Wakaambizana fedha hizo zipelekwe kupitia helikopta ya kampuni walikoshushia mzigo wa saruji na madereva hao wapepee bendera kuonesha wako salama na fedha hizo zidondoshwe.

“Tuliendelea na safari kisha tukapewa chakula aina ya ugali wa mhogo uliokuwa umejaa michanga pamoja na mboga za majani wasiyoyajua na kulazimika kula tu kwa kuwa walikuwa na njaa.

“Tulipomaliza kula chakula tulikaa kupumzika kidogo kwani walikuwa wamemtuma kijana wao aende akanunue unga kwenye kijiji cha jirani. Baada ya muda kidogo kijana yule alirejea huku akitweta na kusema majeshi ya Congo yalikuwa yanakaribia eneo lile.

“Waliposikia vile tukagawanywa kwa waasi Kutokana na taharuki ya viongozi hao, kila mtekaji alipewa madereva wawili mpaka watatu awaongoze na kuanza kukimbia huku watekaji hao wakiwa wametangulia mbele.

“Walionesha kuchanganyikiwa kwa kweli wakaanza kutufokea huku wametushikia mitutu ya bunduki na kila kundi likaenda upande wake. Kwa kuwa wao ndio waliotangulia, tukaanza kutoroka mmoja mmoja mpaka kwenye kundi letu tukabaki wawili mimi na Issa.

Majeshi ya Congo yawasili kwa watekaji

“Tulisikia wakituita kwa lafudhi yao ya kikongo, watanzania kuya (kuja) watanzania kuya (kuja) jitokezeni sisi ni jeshi la DRC tumewaokoa. Sikuamini masikio yangu tulijitokeza na kupewa msaada haraka.

madereva-tekwa-13-001Furaha ya dereva baada ya kukombolewa na kuwasili nchini na kukutana na ndugu zake.

Mmiliki wa kampuni waliyokuwa wakifanyia kazi madereva hao, Dewji alilishukuru jeshi la DRC na Serikali ya Tanzania kwa kuwa naye bega kwa bega katika harakati za kuwaokoa madereva hao na kubainisha kuwa katika tukio hilo, magari ya kampuni yake ya Simba manne yalichomwa moto na hivyo kupata hasara ya Sh milioni 600.

Alisema alikuwa akiwasiliana na waasi hao kila mara wakimtaka atoe fedha hizo ambazo alikuwa tayari kuzitoa lakini alionywa na jeshi la DRC kuwa endapo atazitoa atawajengea tabia ya utekaji zaidi wanajeshi hao.

Aidha, Dewji alisema Serikali ya DRC imemuahidi kuwa itaendelea kuweka usalama kwa wafanyabiashara wa malori nchini humo na kumhakikishia ulinzi wa doria kila kampuni hiyo itakaposafirisha mizigo yake nchini.

“Hiki kilichotokea ni bahati mbaya, tutaendelea na biashara lakini kwa tahadhari. Biashara yangu inagusa watu wengi si kampuni yangu pekee endapo nitasitisha wengi wataathirika.” alisisitiza.

Balozi wa DRC nchini, Jean Piorre Mutamba, alisema tukio hilo limemshtua na kumpa wakati mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa ni balozi mpya aliyewasili nchini hivi karibuni, hivyo alitumia fikra zake zote ili kuhakikisha madereva hao wanaokolewa. Aliwataka madereva hao kuhakikisha wanawasiliana na ubalozi wa DRC kabla ya kuanza safari ili kuwawekea mazingira ya usalama zaidi na kuwafuatilia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Susan Kolimba, aliwahakikishia madereva hao kwamba tukio hilo ni la bahati mbaya na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuwalinda wananchi wake wanaofanya kazi nje ya nchi.

“DRC ni nchi rafiki na tumekuwa tukifanya nao kazi nyingi. Nina imani tukio hili haliwezi kuvunja uhusiano wetu kwani serikali zote mbili zimefanya jitihada kubwa za kuwaokoa madereva hao,” alisisitiza.

Na Leonard Msigwa/GPL

 

Comments are closed.