ADAIWA KUISHI NA MAITI YA MKEWE SIKU 4

PWANI: Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Liswan, mkazi wa Kibaha kwa Mathias mkoani Pwani, anadaiwa kuishi na maiti ya mke wake ndani kwa muda wa siku nne kwa madai kwamba hakufa bali alikuwa amezimia. 

 

Tukio hilo lililoshangaza wananchi na kuwafanya wakusanyike kushinikiza marehemu aliyefahamika kwa jina la mama Halima atolewe ili akazikwe, lilitokea Mei 2 mwaka huu ambapo inaelezwa kuwa, licha ya jitihada hizo mume alikuwa akiweka ngumu.

 

Akizungumza na Amani, mama mkwe wa marehemu ambaye jina lake hakutaka liandikwe gazetini alisema kuwa, mkwe wake alikuwa akiugua na walihamia eneo linaloitwa Misugusugu kwa ajili ya matibabu na maombezi. “Mkwe wangu alikuwa akiumwa kifafa, sasa mume wake ambaye ni mwanangu alimchukua na kumpeleka Misugusugu, huko wanasema kuna nabii ambaye anaponya.

 

“Siku ya Jumapili nilikwenda Misugusugu kumuona mkwe wangu, nilipofika pale nilimkuta amezidiwa lakini wakawa wanamuombea, neno ambalo aliniambia la mwisho alisema mama nimekumbuka mazoezi, nafikiri pale huwa wanafanya mazoezi kwa sababu ni kama kambi, kuna watu wengine tena wanaombewa ila sijajua ni kwa dini ipi ingawa mwanangu ni muislamu.

 

“Baada ya hapo nilirudi nyumbani, ilipofika siku ya Jumatatu mwanangu mmoja wa kike aitwaye Rehema akanipigia simu, akaniuliza kama nina taarifa ya kufariki kwa mama Halima. Nikamwambia sina taarifa.

“Tuliendelea kukaa tu hapa nyumbani kwa kuwa marehemu alikuwa Misugusugu na mume wake na ndiko alikofia, siku ya Alhamisi tukaona gari imekuja na mwanangu pamoja na wenzie, wakamshusha huyo marehemu, wakamuingiza ndani, mimi na ndugu zangu kwa sababu walifika hapa tukataka kuingia humo kwenye hicho chumba, mwanangu akakataa na kusema kuwa mke wake hajafa.

 

“Humo ndani wakawa wanaongea kama watu wanasali hivi, tukaendelea kugonga mlango lakini waligoma kufungua, ndipo majirani walipokusanyika na kuanzisha vurugu na kutulazimu kumuita mjumbe. “Mjumbe alipofika alipiga simu polisi, polisi wapolifika wakagonga lakini hawakufunguliwa, wakabomoa mlango na kukuta mkwe wangu amewekwa kitandani na mwili umevimba hadi inzi wale wa kijani wanasambaa, na kuna harufu kali.

 

“Polisi waliondoka na mwili wakaupeleka hospitali na wakatuambia kuwa marehemu inaonekana amefariki siku nne zaidi kwa ugonjwa wa kawaida, ndugu wakaandika maelezo pale akiwemo mume wa marehemu kisha tukapewa mwili,” alisema mama huyo. Balozi wa Serikali ya Mtaa wa Mwalaka, shina namba 2, Athumani Salumu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema:

 

“Nilipigiwa simu na wananchi wa eneo hilo wakaniambia baba Halima amefunga mlango ili watu wasiingie ndani ikiwa tayari mke wake alishafariki. Ikabidi nipige simu polisi, walipokuja walibomoa mlango na kumchukua marehemu na kwenda naye hospitali kwa ajili ya vipimo kisha tukiwa na familia tulikabidhiwa mwili kwa ajili ya kuuzika lakini ulikuwa umeharibika.

 

“Tulipomaliza kuzika mume wa marehemu aliondoka na baada ya siku mbili akarudi pale nyumbani na kuleta ugomvi kwa familia yake kwa kudai kuwa atawashughulikia kwa kumzika mke wake wakati hajafa, tulishangaa sana.”

Naye mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la mama Monika ambaye alikuwepo kwenye tukio hilo alisema anamshangaa mume huyo wa marehemu kwa kitendo hicho kwani wameshindwa kujua alikuwa na lengo gani.

 

“Siku ya tukio tuliona gari limekuja likamshusha marehemu na kuingia naye ndani, sasa sisi kwa kuwa ndugu zake walikuwa wameshatupa taarifa ya msiba ikabidi twende, tumefika pale majirani wengi tu tukagonga mlango wakawa hawafungui, ndani walikuwa wanaimbaimba, kupika wanapika humohumo ndani na maiti ipo hapo.

 

“Ikabidi tutoe taarifa kwa mjumbe halafu mjumbe akapiga simu polisi wakaja, wakachukua maiti ikiwa imeharibika. “Polisi waliondoka na mwili na baadaye ulirudishwa na kupelekwa kuzikwa, kipindi cha kuzika ulizuka ugomvi, eti mume wa marehemu akawa anadai mkewe hajafa.

 

“Tulibaki tukishangaa tu. Hata hivyo tunashukuru polisi na viongozi wa mtaa ambao walifanikisha mwili huo kuzikwa kwani huenda mpaka leo ungekuwa ndani na hapa mtaani pangekuwa panatisha kwa harufu,” alisema jirani huyo. Jitihada za kuzungumza na mume wa marehemu hazikuzaa matunda kufuatia kutotaka kutoa ushirikiano huku muda wote akionekana mkali kuliko hata pilipili.

BINTI ATESEKA MIAKA 6 KITANDANI/maumivu ya nyonga yalemaza mguu


Loading...

Toa comment