The House of Favourite Newspapers

Agosti 13, Siku ya Watu Wanaotumia Mkono wa Kushoto, Haya ni Maajabu Yao

0
Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama.

Watu wengi duniani hutumia mkono wa kulia kwa shughuli nyingi na si ajabu kwamba vitu vingi huundwa kwa kuwafikiria wanaotumia mkono wa kulia.

Wanaotumia mkono wa kushoto husumbuka sana katika kutumia vitu kama vile mkasi, vitabu au hata kufungua milango.

Fikiria pia kuhusu kipanya katika vituo vya kupokea huduma ya mtandao, mara nyingi utapata kimewekwa upande wa kulia.

Kuna pia viti vyenye sehemu ya kuandikia vyuoni, ni vichache sana hujengwa kwa matumizi ya watu wanaotumia mkono wa kushoto.

Siku ya watu wanaotumia mkono wa kushoto huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Agosti.

Siku hii iliadhimishwa mara ya kwanza mwaka 1976.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Haya hapa ni baadhi ya mambo kumi ya kushangaza kuhusu watu wanaotumia mkono wa kushoto:

  1. Asilimia kumi kati ya watu wote duniani hutumia mkono wa kushoto, na kiwango hiki kimesalia hivyo kwa muda mrefu. Wanaume wana uwezekano mkubwa wa kuwa wanatumia mkono wa kushoto.
  2. Kwa muda mrefu katika jamii nyingi, watu wenye kutumia mkono wa kushoto walichukuliwa kuwa dhaifu. Si ajabu kwamba huenda uliwaona au unawaona watoto wanaochapwa sana kwa kutumia mkono wa kushoto wakila au wakiandika. Katika baadhi ya jamii, kutumia mkono wa kushoto huhusishwa na uchawi.
  3. Kumsalimia mtu kwa kutumia mkono wa kushoto kumekuwa kukitazamwa kama kumkosea mtu heshima. Hii ni kwa sababu watu zamani walikuwa wakitumia mkono wa kushoto kujitakasa baada ya kwenda msalani.
  4. Bingwa wa tenisi duniani Rafael Nadal alibadilisha na kuanza kutumia mkono wake wa kushoto akicheza – kutokana na imani ya mkufunzi wake Toni Nadal kwamba ingempatia nafuu kiasi akikabiliana na wachezaji wengine uwanjani.
  5. Mrengo wa kushoto? Jina hili lilianza kutumiwa miaka ya 1790 baada ya mapinduzi ya Ufaransa na kuondolewa kwa utawala wa kifalme. Wawakilishi wa chama cha kishoshialisto katika bunge walikuwa wakikaa upande wa kushoto wa kiongozi wa vikao. Watu wa mrengo wa kushoto wakati huo walikuwa wakitazamwa kama maadui wa wasomi na watawala.
  6. Kwa muda mrefu, dini ya Kikristo ilihusisha upande wa kushoto na maovu. Kwenye picha nyingi za Siku ya Kiama, wale waovu (mbuzi) hutumwa upande wa kushoto nao wale wa kuokolewa (kondoo) hutumwa upande wa kulia. Wakati wa kusulubiwa kwa Yesu, mwizi aliyetubu alikuwa amewekwa upande wa kulia na yule mwovu alikuwa upande wa kushoto.
  7. Watano kati ya marais wanane wa karibuni zaidi nchini Marekani hutumia mkono wa kushoto kuandika. Marais hao ni Gerald Ford, Ronald Reagan, George H.W. Bush, Bill Clinton, na Barack Obama.
  8. Kuna pahala penye jina Left Hand (Mkono wa Kushoto). Eneo hilo hupatikana katika jimbo la West Virginia na hutokana na kijito cha Lefthand Run.
  9. Katika mchezo wa baseball, jina la ‘southpaws’ hutumika kuwataja wachezaji wanaotumia mkono wa kushoto.
  10. Pete ya ndoa ambayo huvaliwa katika kidole cha tatu cha mkono wa kushoto asili yake ni Ugiriki na Roma ambapo walikuwa wakivaa ili kujikinga na mabaya yaliyokuwa yakihusisha na mkono wa kushoto.
Justine Bieber.

Miongoni mwa watu mashuhuri wanaotumia au waliotumia mkono wa kushoto:

  • Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama
  • Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
  • Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
  • Mwanamfalme William wa Uingereza
  • Msanii Angelina Jolie
  • Mwanasayansi Albert Einstein
  • Mwigizaji Tom Cruise
  • Mwanamuziki David Bowie
  • Mwanariadha Paula Radcliffe
  • Mwanakandanda Pele
  • Mwanaanga za juu Neil Armstrong
  • Mwanasayansi Marie Curie
  • Bondia Manny Pacquiao
  • Mwanaviwanda Henry Ford
  • Mwanamuziki Justin Bieber
  • Mwanamuziki Lady Gaga
  • Mwanamuziki Marshall Bruce Mathers III maarufu kama Eminem
  • Mwanamuziki Paul McCartney
  • Mwigizaji Jennifer Lawrence

Sikio la kushoto

Kwa jumla, watu 40% duniani hutumia zaidi sikio la kushoto kusikia, 30% hutumia jicho la kushoto na 20% hutumia zaidi mguu wa kushoto.

Mabingwa wa tenisi

Ingawa ni asilimia 10% ya watu duniani hutumia zaidi mkono wa kushoto, tangu kuanza kwa enzi ya Open katika mchezi wa tenisi duniani, 23% ya mataji ya Wimbledon ya mchezaji mmoja mmoja yameshindwa na wachezaji wanaotumia mikono ya kushoto.

===

Usipitwe na Matukio, Download na Install ==> Global Publishers App

Leave A Reply