The House of Favourite Newspapers

Air Tanzania Yasitisha Safari za Kwenda Afrika Kusini

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amesema Serikali imesitisha kwa muda huduma ya usafiri wa ndege zake nchini Afrika Kusini hadi hali ya usalama nchini humo itakapotengamaa.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Septemba 5, Kamwelwe amesema ndege hiyo imetua nchini jana saa moja usiku lakini itasitisha safari zake za kwenda Afrika Kusini kwa sasa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo vurugu zinazoendelea nchini humo.

 

“Sababu hizo ni pamoja na usalama wa chombo chenyewe kutokana na hali ya vurugu iliyopo nchini humo hadi pale tutakapohakikishiwa usalama wetu na abiria.

“Wanasheria wamebaki Afrika Kusini wakiendelea kufuatilia hukumu iliyotolewa na kuhakikisha aliyefungua kesi analipa gharama zote,” amesema.

 

Vurugu hizo zilianza Jumapili Septemba Mosi, 2019 baada ya raia wa nchi hiyo kuvamia mitaa yenye maduka ya raia wa kigeni na kuanza kupora mali na kuchoma moto.

Pamoja na mambo mengine, amesema leo asubuhi ndege hiyo imefanyiwa ukaguzi iko salama inasubiri kupangiwa safari ya njia nyingine itakayoanza leo.

Comments are closed.