The House of Favourite Newspapers

Ajibu Aja na Mikakati ya Kibabe Simba SC

BAADA ya Jumamosi iliyopita kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu kuiwezesha timu yake hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bandari FC ya Kenya sasa ameweka wazi mikakati yake anayotarajia kuifanya msimu huu.

 

Ajibu aliifungia Simba bao hilo pekee katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar lakini pia likiwa ni bao lake la kwanza tangu ajiunge na Simba akitokea Yanga katika usajili mkubwa.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Ajibu alisema kuwa sasa ndiyo ameanza kazi na amejipanga kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zake zote zijazo.

 

Alisema kilichokuwa kikimpata tabu hapo mwanzo ni kuingia katika mfumo wa kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems, ila hivi sasa ameshaingia na anaamini atafanya mambo makubwa kuliko alivyokuwa Yanga msimu uliopita.

 

“Namshukuru Mungu sasa mambo yanaenda vizuri jambo ambalo limeniongezea hali ya kujiamini na kuzidi kupambana zaidi.

 

“Changamoto ambayo nilikutana nayo awali ni kuwa majeruhi lakini pia kuingia katika mfumo wa kocha, hivi sasa nishaingia na ni matumani yangu nitaendelea kufanya vizuri zaidi msimu huu pengine kuliko msimu uliopita ili niweze kuiongoza timu yangu kutetea ubingwa wake,” alisema Ajibu.

Stori: Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.