The House of Favourite Newspapers

Ajibu, Kahata wapigwa ‘stop’ Simba

KOCHA Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems amewataka viungo wake kupiga pasi za haraka wakati wakiwa na mpira wakishambulia huku akiwapiga ‘stop’ kukaa na mpira muda mrefu wakipiga chenga zisizokuwa na faida kwa timu.

Hiyo, ikiwa ni baada ya timu hiyo kutua kwenye Mji wa Rustenburg nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya.

 

Timu hiyo, jana ilisafiri kwenda kwenye mji wa Johannesburg nchini humo kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Orlando Pirates uliokuwa unatarajiwa kupigwa saa kumi kamili jioni.

 

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu aliyekuwa kambini nchini huko, kocha huyo yupo mwishoni katika kukifanyia marekebisho kikosi hicho kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.

MBA

Rweyemamu alisema kuwa hivi sasa kocha huyo anamalizia kutengeneza muunganiko mzuri kati ya viungo akiwemo Ibrahim Ajibu, Francis Kahata, Sharraf Shiboub, Mzamiru Yassin na Hassan Dilunga.

Aliongeza kuwa katika mazoezi yake ya siku chache zilizopita kabla kina Ajibu hawajaondoka kocha alionekana akiwapa maelekezo viungo hao jinsi ya kuanzisha na kupeleka mashambulizi golini kwa wapinzani.

 

“Kocha hivi sasa yupo kwenye maandalizi ya mwishoni ya kukiandaa kikosi chake ambacho anataka kuona kabla ya kurejea Dar awe tayari ameshapata kikosi chake cha kwanza.

 

“Katika kikosi hicho anataka kuona wachezaji wake wote wameshika mifumo miwili ya uchezaji aliyopanga kuitumia katika msimu ujao na hataki kuona kiungo anakaa na mpira.

 

“Na uzuri ni kwamba kocha mwenyewe tayari ameridhishwa na viwango vya wachezaji wote wakiwemo wapya na zamani aliokuwa nao kwenye msimu uliopita,”alisema Rweyemamu.

Comments are closed.