The House of Favourite Newspapers

Ajibu kuipatia Simba mil 640

Ajib-mpiraSweetbert Lukonge, Gazeti la Championi Jumatatu, Januari 2, 2017

Dar es Salaam

BAADA ya hivi karibuni mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu kufanikiwa kufanya vizuri katika majaribio ya kucheza soka la kulipwa huko nchini Misri, uongozi wa timu hiyo unajiandaa kupokea mamilioni ya fedha yanayokadiriwa kufikia yale ya Mganda, Emmanuel Okwi alipouzwa katika Klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo yalikuwa ni dola 300,000  (zaidi ya Sh milioni 640).

Ajibu ambaye tayari amesharejea nchini, alikuwa katika Klabu ya Haras El Hodood ya Misri akifanya majaribio ya kutafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa klabuni hapo na inadaiwa kuwa mambo yake siyo mabaya kwani amefanikiwa kuwashawishi baadhi ya viongozi wa timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa akiuonyesha uwanjani.

Mmoja wa viongozi wa Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini, ameliambia Championi Jumatatu kuwa endapo mambo yataenda vizuri, basi klabu hiyo inaweza kulamba mamilioni ya fedha kama yale waliyoyapata kwa Okwi walipomuuza katika Etoile.

Alisema thamani ya Ajibu kwa sasa inafikia mamilioni hayo kwa sababu umri wake bado ni mdogo lakini pia kiwango chake cha kutandaza soka ni cha hali ya juu, hivyo wanaamini kabisa endapo wataiambia Haras El Hodood itoe kiasi hicho cha fedha, bila shaka inaweza kutoa.

“Hata kama wakigoma na kushuka kidogo chini ya hapo siyo mbaya kwani tutapata fedha nzuri pia kuliko akiondoka bure klabuni kwetu,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Simba, Haji Manara, alisema: “Sina taarifa yoyote kuhusiana na hilo, lakini pia ni mapema sana kulizungumzia hilo kwa sababu bado hatujapata taarifa yoyote rasmi kutoka katika timu hiyo kuhusiana na majaribio yake.

“Taarifa ambazo tumekuwa tukizisikia ni zile za kwenye mitandao kuwa amefuzu, hivyo sisi hatuwezi kufanya maamuzi yetu kwa kufuata taarifa za mitandaoni isipokuwa kila kitu tutakifanya baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka katika klabu hiyo.”

Kwa upande wake Ajibu alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, hakutaka kuzungumza chochote zaidi ya kuitikia tu kila alichoulizwa kisha akakata simu na kuizima.

Comments are closed.