The House of Favourite Newspapers

Akili Za Kiuswahili Zimeiingiza Simba Kwenye Matatizo

Kikosi cha timu ya Simba.

SIMBA imeingia kwenye matatizo. Tena matatizo kwelikweli. Akili walizoingia nazo kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Green Warriors zitawagharimu.

Zitavuruga kabisa upepo pale Msimbazi. Kama huamini endelea kusubiri. Hawakuuchukulia mchezo huo katika umuhimu stahiki, hilo lilianzia kwa wachezaji mpaka na viongozi wenyewe matokeo yake wakatema kombe la FA.

Timu ya daraja la pili imedhalilisha kikosi cha mamilioni, hapo ndipo unapoambiwa kwamba mpira ni mipango siyo majina wala maneno.

 

Simba wana kila kitu lakini waliingia uwanjani Kiswahili na Warriors wakatembea nao kindava sana. Simba walichukulia mambo rahisi sana bila kujua kwamba na wenzao wanalitamani dirisha dogo ambalo lilifungwa jana. Huwezi kucheza mechi muhimu kama ile tena ukiwa bingwa mtetezi na kikosi cha kawaida, ni dharau na Uswahili ambao saa nyingine tunaupeleka mpaka kwenye maisha ya kawaida uraiani. Watu hawaweki umuhimu kwenye mambo ya msingi. Uswahili unakuwa mwingi sana.

 

Mpira haujawahi kuwa rahisi kiasi hicho, lazima mjifunze. Walichokifanya Simba juzi pale Chamazi kitawagharimu kwelikweli kwavile wamejiingiza kwenye nafasi finyu ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa msimu ujao.

 

Walidhani kwamba Warriors ni timu laini ambayo wanaweza kumaliza mchezo dakika 90 ndio maana wakapanga kikosi cha kawaida, lakini upepo ulipowabadilikia wakachanganyikiwa na mchezo ukawa mgumu kwao.

 

Warriors hawakucheza mpira mkubwa sana walichofanya wao ni kuivuruga akili Simba, ikaamua kuwakamata Kichuya, Muzamiru, Mkude na Bocco. Na walikuwa wanatembea nayo mguu kwa mguu wakatibua hali ya mchezo. Yaani ilikuwa mchezaji wa Simba apotee njia na mpira ubaki.

 

Mpira unahitaji nidhamu ya hali ya juu sana, Warriors kila walipokuwa wakitua kwenye miguu ya wachezaji wa Simba waliwashinda kisaikolojia. Na kupaniki kwa Simba kulikuwa kunawafanya wanapoteza mipira bila sababu za msingi kabisa, walipoteana na walikubali kutawaliwa na timu ndogo ya Daraja la Pili.

 

Kinachotokea sasa ni kwamba Simba amepoteza turufu ya muhimu sana, nafasi ya kupata tiketi ya kimataifa ukiwa kwenye FA na Ligi ni kubwa lakini kinachotokea sasa ni kuwa Simba imesaliwa na upenyo mmoja tu ambao ni Ligi.

 

Hilo ndilo litakalotoa upenyo kwa wanafiki kuanza kuzalisha matatizo.. wataanza kutafuta matatizo kila kona kuanzia kwa kocha, wachezaji mpaka kwa uongozi.

 

Kwenye Ligi ni pagumu. Simba iko kwenye presha mbili. Kwanza kuchukua ubingwa ili kurejesha heshima yake iliyopotea siku nyingi, lakini vilevile kupata nafasi ya kushiriki kimataifa msimu wa 2019.

Lakini sasa hilo haliwezi kuwa rahisi, inahitajika nguvu kwelikweli. Msimu huu timu nyingi kwenye ligi zimejipanga ingawa mchuano unaoonekana kwa karibu na mashabiki ni ule wa Simba dhidi ya Yanga, Singida, Mtibwa na Azam.

 

Ndio maana naona ugumu Simba iliyojitafutia kutokana na kufikiria mambo kirahisi tu. Huwezi kumshawishi shabiki au mwanachama akuelewe pale kikosi cha Shilingi bilioni moja kinapofanya makosa ya kizembezembe na kuvurugwa na timu zenye miundombinu ya kawaida kabisa kama Warriors.

 

Simba wanahitaji kujipanga na kuchukulia kila kitu kwa umuhimu wake, kipigo cha Warriors ni aibu na fundisho kubwa kwamba soka halichezwi mdomoni, mpira ni uwanjani. Haujifichi. Tuache kufikiria Kiuswahili swahili.

Stori na Michael Momburi | Spoti Xtra

Comments are closed.