The House of Favourite Newspapers

Hellen Dausen Alichomwa Jua, Akakatishwa Tamaa, Sasa Anaishi Ndoto Zake!

Mrembo Hellen Dausen.

 

MREMBO Hellen Dausen ni mshindi wa kinyang’anyiro cha Miss Universe 2010. Ni miongoni mwa wajasiriamali na wanadada wa chuma nchini ambao taifa linawatazama mbali sana.

 

Anamiliki bidhaa zenye brandi ya Nuya’s Essence ambazo ni sabuni za kuogea, mafuta mepesi ya kupaka, mafuta halisi ya nazi, ‘body scrub’ na manukato.

 

Mwaka 2016, Jarida la Forbes Africa lilimtaja mrembo huyu kuwa miongoni mwa Waafrika wenye umri chini ya miaka 30, wanaotarajiwa kuwa mabilionea miaka michache ijayo.

Baada ya taarifa hiyo, gazeti dada wa hili Ijumaa Wikienda, lilimtafuta Hellen na kuzungumza naye mambo mengi juu ya wapi alipoanzia mpaka hapo alipofika.

 

Alieleza kwamba, haikuwa safari ndogo kupigania ndoto zake, ilimpasa kupitia mabonde na milima mpaka kufikia kilele cha matamanio ya mafanikio yake.

 

Takribani miaka miwili imekatika tangu tuzungumze naye mwezi Julai, 2016, huyu hapa Ijumaa imemleta kwako kwa mara nyingine uweze kufahamu nini kinaendelea kwenye biashara yake.

IJUMAA: Hellen tunaomba uwakumbushe wasomaji wetu umezaliwa kwenye familia ya namna gani na umekulia wapi?

HELEN: Nimezaliwa kwenye familia ya kawaida na nimekulia Mitaa ya Makumbusho na Kijitonyama, Dar.

IJUMAA: Vipi kuhusu elimu yako?

HELLEN: Kuhusu elimu, shule ya msingu nilisoma Muhimbili na sekondari nilisoma Shule za St. Mary’s kwa elimu ya awali na baadaye Shaabani Robert zote za jijini Dar. Nilipomaliza masomo ya sekondari nilijiunga na chuo cha United International University kilichopo Kenya kwa masomo ya biashara ambapo nilichukua digrii.

IJUMAA: Kipindi cha mwisho tumezungumza ulitaja kuwa na bidhaa aina nne, sasa zimefika ngapi?

HELLEN: Zipo aina tofautitofauti 30, ambapo ni zile za mwanzo na nyingine mpya. Kwa jumla tuna sabuni za kuogea, mafuta mepesi ya kupaka, mafuta halisi ya nazi, body scrub na manukato. Kikubwa zaidi tumeongeza pia harufu mbalimbali kwenye kila bidhaa.

IJUMAA: Kibiashara umejikita wapi na vipi kuhusu serikali, inakupa sapoti?

HELLEN: Kibiashara nipo Zanzibar toka mwaka 2014. Kuhusu serikali kiukweli inanipa sapoti, vibali ninapata kwa muda na hakuna usumbufu wowote ambao ninapata.

IJUMAA: Nini hasa changamoto ambazo unakumbana nazo kwenye biashara yako?

HELLEN: Unajua kila hatua unapopiga kwenye biashara unakuta kuna changamoto tofauti. Kwa mfano wakati ninaanza changamoto kubwa ilikuwa ni kupata mtaji na kuongeza mtaji kwenye biashara yangu. Lakini namshukuru Mungu mwaka 2016, nilijiunga kwenye mashindano ya mawazo ya kibiashara huko Marekani, nikashinda na kupata mtaji wa kuweka kwenye biashara yangu.

Hata hivyo changamoto kubwa kwangu kwa sasa ni malighafi. Inanilazimu kuagiza malighafi nje kwa sababu hapa nyumbani kuna aina chache za mafuta na unakuta hayasafishwi vizuri, sasa ili niweze kupata mafuta ambayo yataniwezesha kutengeneza bidhaa bora inanilazimu kuagiza nje.

IJUMAA: Unawashauri nini vijana wanaotarajia kuingia kwenye biashara au wapo kwenye biashara lakini wanakutana na changamoto mbalimbali?

HELLEN: Kikubwa wasikate tamaa. Unajua tatizo vijana wengi siku hizi wanapenda mafanikio ya papo kwa hapo. Wakianzisha biashara mwaka mmoja na kuona mambo hayaendi wanakata tamaa na kuachana nayo. Watu wawe wavumilivu, kama changamoto ni mtaji kuna njia nyingi za kuongeza mitaji. Kuna mashindano mbalimbali juu ya mawazo ya biashara huko mitandaoni wanaweza kushiriki na wakapata mitaji.

IJUMAA: Uliwahi kuzungumzia kujenga kiwanda, vipi umefikia wapi?

HELLEN: ‘Process’ zinaendelea, ni ndefu lakini nimefika mahali pazuri, namshukuru Mungu kwa hilo. Nitakamilisha tu.

IJUMAA: Kwa sasa umeajiri watu wangapi?

HELLEN: Nimeajiri watu kumi na tano ambao wapo kwenye maduka mbalimbali. Lakini kuna wengine ambao tunashirikiana nao kwa kazi zinazojitokeza ‘part time’.

IJUMAA: Ni mfanyabiashara gani anakuvutia nchini?

HELLEN: Kiukweli sijawahi kuwa makini na hilo, inabidi nipate muda zaidi wa kulifikiria.

IJUMAA: Kuna makampuni ambayo unashirikiana nayo kibiashara?

HELLEN: Ninashirikiana na makampuni binafsi kama 20. Wapo watu wananiletea mafuta, wasanii mbalimbali wanaobuni na kutengeneza bidhaa zetu, watu wanaodurufu, watu wanaopaki bidhaa zetu, kiukweli ni watu mbalimbali tunafanya nao kazi.

IJUMAA: Mwisho kabisa una kipi cha kumweleza kijana mwenye ndoto anayehitaji kuzitimiza.

HELLEN: Kwanza kabisa anatakiwa kufahamu ndoto aliyonayo amepewa mwenyewe. Amepewa kwa sababu Mungu alifahamu yeye ndiye mtu sahihi wa kuitimiza. Kwa hiyo ainuke na kupambana bila kumsubiri yeyote yule kuwa nyuma yake
Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.