The House of Favourite Newspapers

Aliens; bado tishio jipya duniani!

0

aliensETLIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita nilieleza jinsi ambavyo kwenye miaka ya hivi karibuni, neno UFO (Unidentified Flying Objects) limechukua kasi hasa nchi za Magharibi, Asia na nyinginezo. Taarifa zisizokuwa rasmi zinadai UFO ni vyombo vya angani kama ndege za ajabu vinavyotumiwa na Aliens ambavyo tabia zake ni tofauti sana na vyombo vyetu vya anga.

SASA ENDELEA…

Kuna dhana nyingi mno katika ishu hii ya Aliens. Je, wewe unaamini humu duniani tunaishi wenyewe bila viumbe wengine? Swali hilo lina majibu mengi na tofauti, nitayaangazia huko mbele.

Wakati Wamarekani wakiwa katika kitisho hicho cha uvamizi wa Aliens, Machi 13, 1997, Jimbo la Arizona nchini Marekani lilishuhudia kile ambacho baadaye kilijulikana kama ni UFO. Baada ya tukio hilo, simu zilimiminika kwenye vituo vya dharura vya jimbo hilo kutoka kwa mashuhuda wa maeneo kadhaa ikiwemo Prescott, Wickenburg, Glendale, Phoenix, Scottsdale na Tempe.

Chombo hicho chenye kung’aa na kutoa mwanga mkali kilikuwa karibu kabisa na Kituo cha Luke Air Force, ndege tatu aina ya F-16, zilizotoka kwenda kukifuatilia chombo hicho kujua kulikoni.

Ndege za kijeshi za Marekani ziliruka kukifuata chombo hicho kilichokuwa kikielea angani na zilipokikaribia, kilitoweka ghafla kama kupepesa mboni ya jicho. Baadaye maafisa wa kituo hicho walikanusha kuwa hakuna ndege za kijeshi zilizotolewa kwenda kukifuatilia chombo hicho na wala hawafanyi tafiti juu ya UFO.

Peter Davenport kutoka kwenye kituo cha taifa cha kutoa taarifa za UFO kilichopo Seattle, Washington alipokea mamia ya simu kuhusiana na tukio hilo na maoni yake binafsi ni kuwa: “Tukio la Arizona lilikuwa la wazi kabisa kati ya matukio niliyopata kuyaona… tulichokiona pale ni kitu cha kweli kabisa. Tayari wako hapa (viumbe kutoka sayari nyingine).”

Tukio hilo lilikuwa gumzo kwenye vyombo vya habari huku likipata mvuto wa aina yake. Kilichoonekana, watu wengi walitaka kujua habari hizo zilizovuta hisia za wengi.

Shuhuda mwingine, Mike Fortsen ambaye alishuhudia tukio hilo kwa macho alisema: “Nina uhakika kabisa na kushawishika kuwa kile kilikuwa ni chombo cha viumbe kutoka kwenye ulimwengu mwingine.”

Ifahamike kwamba, dunia tunayoishi sasa ni maarufu kama ‘pande tatu’ au ‘miwanda mitatu’. Miwanda ni wingi wa uwanda. Wanaita ‘Three Dimensional au 3D’!

Tukio hili la Arizona liliripotiwa kwa undani kwenye Gazeti la USA Today katika ukurasa mzima. Kwenye makala hiyo, mwandishi na mtafiti Richard Price aliliita tukio hilo: “Tukio la ajabu na kushangaza la UFO tangu miaka 50 iliyopita.”

Alisema kuna kitu kimetokea kwenye anga la Arizona na hakuna mwenye uhakika wa kwamba kilikuwa ni kitu gani, lakini maelfu walikiona na kukirekodi kwa njia ya video na watu kwenye jimbo zima.

Mashuhuda wa tukio hilo walikubaliana kwenye vitu vitatu juu ya tukio hilo. Kwanza, chombo chenyewe kilikuwa kikubwa mno. Makadirio ya karibu ni kuwa ukubwa wake ulikuwa ni sawa na urefu wa viwanja vitatu vya mpira wa miguu halafu kikawa kinaelea angani, jambo lililotia hofu na kushtua wengi.

Uchambuzi wa kompyuta kupitia video zilizorekodiwa ulikadiria kuwa ni sawa na futi 6,000 au zaidi ya maili moja ikielezwa kuwa chombo hicho hakikutoa kelele yoyote, kilikuwa kimya kama hakipo.

Leave A Reply