The House of Favourite Newspapers

Hizi Hapa Sababu za Kwa Nini Mpenzi Wako Hakuonei Wivu?

MAPENZI yananoga wivu unapokuwa ndani yake. Ukitathimini kwa harakaharaka, unaweza kusema kama hakuna wivu, hakuna mapenzi. Inapotokea mpenzi wako, hata ufanye nini hakuonei wivu, bila shaka hata wewe utahisi kuna tatizo.

 

Unatamani kale ‘kawivu’ kidogo ili ujisikie unapendwa. Maana, tafsiri nyingine ya mtu asiyekuwa na wivu, huwa ni ile ya ‘wewe fanya yako, na mimi nifanye yangu. Tusiingiliane!’

Wivu unapozidi kipimo, nalo huwa ni tatizo lingine. Tunakubaliana hakuna ambaye anafurahia kusalitiwa. Usaliti unauma. Hakuna ambaye atafurahia pindi asikiapo mwenzake amemsaliti. Ndiyo maana wapendanao hutumia nguvu nyingi sana kuhakikisha tu mwenzake hamsaliti.

 

Wapo ambao wanadiriki hata kuwawekea ulinzi wenza wao ili kuhakikisha kwamba kila kitakachofanywa na mpenzi wake anakijua. Kila eneo atakapokuwa mpenzi wake kunakuwa na watu wanaofikisha habari kama zilivyo.

Kundi la wanaume au wanawake wa aina hiyo ndiyo wale wanaokosa ustahimilivu. Akimuona mpenzi wake amesimama na mtu tu barabarani, hana imani. Anatamani kujua wanazungumza nini. Mpenzi wake akichelewa kurudi nyumbani, anatilia shaka.

 

Anapiga simu kila dakika. Anamuuliza yuko wapi. Ikiwezekana amfuate hapo alipo ili kama kuna figisufigisu zozote azifumanie. Akiwa amekaa pamoja na mpenzi wake anakosa amani. Simu ya mpenzi wake ikiita, anatega sikio haraka kusikiliza anayezungumza naye ni nani. Huo ndio wivu uliopitiliza.

Kukagua simu kila wakati. Anataka kuona kama kuna madudu. Kila wakati anawapigia marafiki wa mpenzi wake, kujua taarifa za mtu wake. Hiyo ndiyo staili ya maisha yake. Matokeo yake inageuka kero kubwa kwa yule anayefuatiliwa.

 

Hapo ndipo zinapoibuka kauli kama hizi; “Huyu naye amezidi bwana. Haiwezekani awe ananichunga kama mbuzi. Mimi ni mtu mzima. Najua mema na mabaya. Bora hata ingekuwa kweli nafanya madudu lakini sifanyi. Yeye kila siku ananifuatilia.

“Nakosa uhuru. Kila unachofanya unajua unafuatiliwa. Kila ukifanya kitu anakitilia shaka. Bora hata tuachane maana kwa staili hii tutakuwa watu wa kugombana kila kukicha.”

PENZI BORA HUJENGWA NA IMANI

Marafiki zangu hapa kuna kitu cha kujifunza. Kuna umuhimu mkubwa wa kuishi na mtu unayemuamini. Mwanadamu huwezi kumchunga. Kama mtu una shaka naye ni bora kuachana naye.

Kila mmoja wenu anapaswa kujitambua. Akili ya kujitambua kila mwanadamu amepewa na Mungu. Kutambua wewe ni nani na huyo uliyenaye mna malengo naye gani? Jadilini pamoja kuhusu umuhimu wa kujitambua na kila mtu aishi kulingana na matakwa yenu mliyoyachagua.

Kama mna malengo ya kuishi kama mke na mume, heshima ya mume na mke ni nini? Mume ajitambue kwamba anapaswa kulinda utu wa mwenzi wake, vivyo hivyo kwa mke. Hakuna kinachobadilika kwenye mapenzi. Kila unachokihitaji kwa maana ya mahitaji ya kimwili, kiakili na hata kifikra, mpenzi wako anacho.

ONGOZWENI NA MALENGO

Tangulizeni malengo au nia ya uhusiano wenu mbele. Hakuna sababu ya kuwa na tamaa. Ridhika na kile unachokipata kutoka kwa mpenzi wako. Uone kwamba unaposaliti ni kama mpenzi wako anakuona unachokifanya. Utambue kwamba kuna maradhi pia. Kama unampenda kweli kwa nini umsaliti? Mnapaswa kukubaliana kwamba hakuna sababu ya kuchungana lakini kila mmoja wenu ajichunge mwenyewe.

Njia ya muongo siku zote ni fupi. Huna sababu ya kumchunga sana mpenzi wako kwani ipo siku ataumbuka yeye mwenyewe. Ikitokea hivyo mtazungumza na akiomba msamaha na kuahidi kutorudia, msamehe na umpe nafasi nyingine.

MWANADAMU HACHUNGWI

Nisisitize kwamba hakuna sababu ya kuchungana, kila mmoja ajichunge mwenyewe kwa kujiwekea uaminifu kwa mwenzake!

Comments are closed.