The House of Favourite Newspapers

ALIYEDAIWA KUUA MKE, MTOTO KWA JEMBE HUYU HAPA KORTINI!

Ammy Lukule akipelekwa mahakamani.

 

DAR ES SALAAM: MKAZI wa Goba Matosa, Ammy Lukule (49), aliyedaiwa kumuua mkewe, shemeji yake na mtoto, amewahenyesha askari alipokuwa akipandishwa kizimbani juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam kisha kusomewa mashtaka matatu ya mauaji yanayomkabili.

 

Mtuhumiwa huyo aliwahenyesha askari magereza kwani wakati akiingia muda wote alikuwa akiwasumbua kutaka kujua kama kuna ndugu zake wamefika mahakamani hapo kitu ambacho kiliwachosha askari magereza.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina, Wakili wa Serikali, Masini Musa, alidai kwamba mtuhumiwa ambaye ni mhasibu kutoka Hospitali ya Rufaa mkoani Mbeya, alitenda kosa hilo Januari 4, mwaka huu nyumbani kwake Goba-Matosa.

Waliouawa, Mke (kushoto) na mdogo wake.

Katika tarehe tajwa wakili huyo alidai kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kumuua Pendo Makale (mkewe), pili, alimuua Magreth Samwel (shemeji yake) na shtaka la mwisho analokabiliwa ni kosa la kumuua mtoto wake aitwaye Joshua Ammy.

“Ulitenda kosa hilo kinyume cha kifungu sheria namba 196, cha mwenendo wa makosa ya jinai kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alidai wakili Musa.

 

Baada ya kusomewa maelezo ya makosa hayo, wakili alidai upelelezi bado haujakamilika ambapo Hakimu Mhina alisema mtuhumiwa hawezi kudhaminiwa pia hapaswi kujibu kitu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hadi upelelezi utakapokamilika ambapo itasikilizwa Mahakama Kuu.

 

Wakati mtuhumiwa huyo akitoka mahakamani hapo baada ya kusomewa mashtaka hayo alipofika nje, ndugu yake mmoja alikuwa akimuuita kwa sauti lakini hakutaka hata kumuangalia wala kumsikiliza.

Mtuhumiwa amerejeshwa mahabusu hadi Machi 20, mwaka huu kesi itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Stori: Imelda Mtema, Amani

 Stori: Richard Bukos, Amani

“JPM Nisaidie, Nasubiri Kifo Tu!” – Mama Shimeda (Video)

Comments are closed.