The House of Favourite Newspapers

“JPM Nisaidie, Nasubiri Kifo Tu!” – Mama Shimeda (Pichaz + Video)

Hali ya mguu wa Beatrice Shimeda.

 

DAR ES SALAAM: MKAZI wa Kibamba Kwembe Jijini Dar, Beatrice Shimeda (54) analia na mateso ya mguu wake tangu mwaka 1997 hivyo kutimiza miaka 21 ya mateso hayo ambapo sasa anawaomba Watanzania wenye moyo wa huruma wamsaidie ili aweze kwenda India kutibiwa kwani vinginevyo atasubiri kifo tu.

 

Akizungumza na gazeti hili, Beatrice alisema chanzo cha tatizo hilo ilikuwa ni kama mauzauza ambapo alianza kusimulia;

“Siku hiyo nilikuwa Kimara kwenye biashara yangu ya saluni nikashtukia kitu kama kimenichoma kwenye paja upande wa nyuma kisha kikanichoma tena kwa mbele.

“Nilikitafuta hicho kitu kilichonichoma lakini sikukiona hivyo nilidharau, muda ulipofika nilirudi nyumbani ambapo niliumwa na homa kali sana.

Beatrice Shimeda alivyokuwa kabla ya kupelekwa India.

 

“Nilikimbizwa hospitali nilipofika nilitundikiwa dripu tatu za maji lakini cha ajabu maji yote yalikimbilia kwenye huu mguu ambao ulianza kubabuka na kuvimba sana.

“Nilihangaika hospitali mbalimbali hapa nchini lakini mguu wangu ulizidi kuvimba na kufikia uzito wa kilo 79 huku ukiniuma sana,” alisema mama huyo.

 

Baada ya hali kuwa mbaya sana, mama huyo anasema mwaka 2014 alipelekwa Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu kwa msaada wa serikali ambapo alifanyiwa upasuaji na kuwekwa vyuma na vitu vingine ndani ya nyama za mguu huo na kushauriwa arudi tena mwaka 2015 ili aondolewe vitu hivyo.

Beatrice alisema ilipofika mwaka 2015 alipoenda tena serikalini kukumbushia safari yake ya kurudi India, aliambiwa asubiri uchaguzi upite na ulipopita aliambiwa serikali imesitisha utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Baada ya kusitishiwa safari ya kurudi nchini India, Beatrice alianza kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini mguu huo umeanza kuvimba tena na kutoa maji huku maumivu yakizidi kuwa makali.

Kabla ya kuwekewa vyuma.

Beatrice aliendelea kusema: “Kuna vitu niliwekewa India ambapo madaktari wa huko waliniambia inabidi ukifika muda niende wakanitoe lakini ndiyo hivyo tena safari zimesitishwa na madaktari wa hapa nikiongea nao wanasema hawana utaalamu wa kuvitoa labda wanikate mguu.

“Wanasema kwa wao sasa hawaruhusiwi kutoa vibali vya kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa gharama ya serikali labda nijitegemee mwenyewe nami sina uwezo wa kujigharamia safari ya kwenda huko.

 

“Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu wenye moyo wa huruma mnisaidie michango ya hali na mali ili niweze kurudi India nikatolewe vitu nilivyowekewa ndani ya mguu na kumalizia upasuaji sehemu iliyobaki ili niweze kuondokana na maumivu makali na kifo. Namuomba sana Rais wangu, Dk John Pombe Magufuli aniangalie kwa jicho la huruma.

Beatrice Shimeda enzi akiwa mzima wa miguu yote.

 

“Gharama zote za kwenda na kurudi pamoja na matibabu nimewasiliana na uongozi wa hiyo hospitali wameniambia ni dola za kimarekani elfu 23 (sawa na takribani shilingi milioni 53).”

Beatrice alimalizia kwa kuomba kama kuna msamaria mwema mwenye moyo wa huruma awasiliane naye kwa namba ya simu 0652444188.

 

 Stori: Richard Bukos, Amani

TAZAMA VIDEO MAMA HUYO AKILIA MGUU WAKE

Comments are closed.