The House of Favourite Newspapers

Aliyedaiwa Kuuawa na Mumewe Aibuka!

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa Kijiji cha Mwibagi kilichopo Kata ya Kyanyari, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, wamepigwa na butwaa baada ya mwanamke mmoja, Roza Fungwa (46), aliyedaiwa kupigwa na kuuawa na kuzikwa kusikojulikana na mumewe Fungwa Busia (47) miezi miwili iliyopita, kuibuka akiwa hai na mwenye afya njema.

Mwanamke huyo alirejea kijijini hapo June 23, saa 2.30 za usiku na kuwafanya wananchi wengi wamiminike kwenda kumshuhudia huku wakiwa hawaamini macho yao hasa baada ya kumuona akiwa hai ikiwa ni baada ya kufanyiwa matanga kwa kuamini kuwa amefariki dunia.

Mara baada ya kufika kijijini hapo, mama huyo alichukuliwa hadi kituo cha polisi ambacho mumewe alikuwa amewekwa ndani na alipofika huko alieleza mazito yaliyomfika.

Alidai kuwa, baada ya tukio lililotokea Aprili Mosi, mwaka huu la kupigwa vibaya, alipozinduka ilibidi aondoke na kwenda kwa ndugu yake anayeishi Ukerewe mkoani Mwanza ili kujiokoa na kifo.

Awali, wananchi wa Kijiji cha Mwibagi walimtuhumu mume wa mwanamke huyo, Fungwa Busia kuwa alimpiga mkewe huyo kwa siku mbili mfululizo na kumuua kisha kwenda kumzika kusikojulikana ambapo jeshi la polisi lilimtia mbaroni mtuhumiwa huyo.

Kufuatia mazingira hayo, wananchi wa kijiji hicho waliingia kazini kutafuta eneo ambalo mwanamke huyo alikuwa kafukiwa na mumewe, wakaingia kila kichaka, kila msitu lakini hawakuambulia kitu.

“Tulimsaka sana lakini hatukufanikiwa kuuona mwili wake, wapo walioamua kwenda kwa waganga na kuambiwa kuwa mama huyo alikuwa kauawa na kutumbukizwa chooni, wengine wakasema yupo, kuna siku atarejea,” alisema Judith Kambone, mmoja wa majirani wa mama huyo.

Hata hivyo, baada ya kukaa muda mrefu, wengi waliamini kuwa, mwanamke huyo alikuwa ameshafariki hivyo ndugu, jamaa na marafiki waliweka matanga na kuyaanua, wakabonoa nyumba ya Fungwa na kuchukua kila kitu kisha watoto wakatawanywa kwa ajili ya malezi.

Baada ya mama huyo kuibuka na kupelekwa polisi, mume wake aliachiwa na wakarejea nyumbani ambapo inaelezwa kuwa, mume alikuwa akiomba yaishe na ndoa yao irejee kama zamani. Akizungumza na Uwazi mara baada ya kutoka polisi, Fungwa alisema:

“Kiongozi wa kusambaza habari za kwamba nimemuua mke wangu ni shemeji yangu, mimi nimesamehe ila ninachotaka shemeji huyo amfanyie tambiko dada yake kwa vile tayari walikuwa wamemfanyia matanga wakiamini amefariki na pia wanirudishie mabati yangu,” alisema.

 

STORI: GREGORY NYANKAIRA, UWAZI


Comments are closed.