The House of Favourite Newspapers

Aliyesota Muhimbili Kisa Laki 2… Achangiwa Sh. 800,000

0

Na Imelda Mtema, UWAZI

DAR ES SALAAM: Katika toleo lililopita la gazeti hili liliandika habari ya kijana Noel Lazaro (26), mkazi wa Kijiji cha Mangamba mkoani Mtwara ambaye aliteseka kwa muda wa miezi miwili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kukosa shilingi 200,000 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Sasa tayari Watanzania wamemchangia shilingi 800,000 kijana huyo kwa ajili ya matibabu na kujikimu akiwa hospitalini hapo.

Akizungumza kwa furaha na gazeti hili, Noel alisema kwamba alikuwa akipata wakati mgumu kila alipokuwa akiamka na kuona hakuna matumaini ya kuweza kufanyiwa upasuaji kwa kuwa hakuwa na kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya kulipia upasuaji huo lakini baada ya  habari zake kuchapishwa na gazeti hili kwa kichwa cha habari; Kijana: Nitafia Muhimbili kwa kukosa 200,000, wasamaria wema walijitokeza kumpa pesa hiyo mpaka kupita kiwango alichokuwa akikihitaji.

 “Yaani sasa hivi nina amani sana na ninamshukuru sana Mungu kwa kunijalia kupata watu ambao wamejitokeza kunichangia. Pia shukurani zangu za dhati kwa mama mmoja aliyekuja mpaka hospitalini siku ya kwanza kabisa, akajitambulisha kwa jina la Catherine Ambakyse ‘Mama Loraa’.

“Huyu mama aliniletea msaada wake wa moja kwa moja, shilingi laki mbili. Mungu awabariki wote walioguswa na mimi, pamoja na uongozi wa Gazeti la Uwazi,” alisema kijana huyo.

Mwaka jana Noel alipata ajali ya Bajaj akiwa mjini Mtwara ambapo alivunjika mgongo hivyo kumfanya ashindwe kutembea na kusimama na akapelekwa katika Hospitali ya Ligula ambapo walimpa rufaa ya kwenda kutibiwa Muhimbili.

Alipokwenda hospitali aliwekewa vyuma  alivyodumu navyo kwa miezi sita na aliporudi tena hospitali vilihitajika kutolewa lakini hakuwa na uwezo wa kulipia gharama ya upasuaji wa shilingi laki mbili.

Leave A Reply