The House of Favourite Newspapers

Ally Niyonzima: Nina Dawa ya Kagere

0

KIUNGO mkabaji wa Rayon Sports ya Rwanda, Ally Niyonzima, ametamba kuwa kwake hakuna straika yeyote anayemhofi a akiwemo mshambuliaji tegemeo wa Simba, Meddie Kagere akisema kuwa anamfahamu vizuri na ana dawa yake.

 

Kagere ndiye mshambuliaji tishio zaidi kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara, msimu uliopita alikuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 23 na tayari msimu huu anaongoza akiwa na mabao 19 wakati ligi ikiwa haijamalizika. Tangu atue kuichezea Simba msimu uliopita, ameshaifunga Yanga mabao mawili.

 

Ally Niyonzima juzi alithibitisha kufanya mazungumzo na mmoja wa viongozi wa Yanga kutoka Kampuni ya GSM iliyochukua jukumu la kufanikisha usajili kwenye msimu ujao wakisaidiana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Luc Eymael na viongozi.

GSM hivi sasa ipo kwenye taratibu za kukamilisha usajili wa staa huyo wa Rayon na washambuliaji wa Horoya AC, Heritier Makambo, Michael Sarpong ambaye ni mchezaji huru, winga wa AS Vita, Tuisila Kisinda na beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ally Niyonzima alisema anafahamu vizuri uwezo wa Kagere kutokana na kuwepo pamoja kwenye timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavumbi’, hivyo hana hofu mara watakapokutana kwenye dabi.

 

Niyonzima alisema kuwa pia mshambuliaji huyo aliwahi kukutana naye mwaka 2019 katika mchezo wa Simba Day, yeye akiwa anaichezea Rayon, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Aliongeza kuwa katika mchezo huo, pia alipambana na nahodha wa Simba, John Bocco, yeye akicheza namba sita katika mchezo huo, hivyo hana hofu mara watakapokutana na washambuliaji hao.

 

“Mara nyingi nimekuwa sipendagi kumzungumzia mchezaji mmoja, lakini kwa sababu umeniuliza nikueleze kuwa, kutokana na nafasi ninayoicheza lazima nitakutana na Kagere, hivyo nikwambie kuwa kwangu sijawahi kumuogopa mchezaji.

 

“Uzuri ni kwamba huyo Kagere ninamjua vizuri, nimekutana naye mara zote tukiwa katika timu ya taifa ya Rwanda, ni mchezaji mzuri na ninaheshimu uwezo wake wa uwanjani, lakini simuogopi kwani ninafahamu uwezo wake.

 

“Ninaamini kama nikija kujiunga na Yanga, amini kuwa hatanisumbua kabisa kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, tutafanikisha malengo yetu ya kutompa nafasi ya kucheza kabisa mara tutakapokutana uwanjani,” alisema Niyonzima.

 

Kiungo huyo mara baada ya kutua, anahitaji kuonyesha ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na uwepo wa viungo Mkongomani Papy Tshishimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Juma Makapu.

STORI: WILBERT MOLANDI NA IBRAHIM MUSSA

JOSEPH MSUKUMA: HAMAHAMA YA WABUNGE | RAIS MAGUFULI 2020 | 255 FRONT PAGE

Leave A Reply