AMBER LULU AIBU 100%

UNAPOAMBIWA msanii ni kioo cha jamii siyo kwa kufanya mambo maovu au kinyume na maadili ya Kitanzania! Msanii na muuza nyago kwenye video za Kibongo, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ amefanya tukio la aibu 100% ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.

TUJIUNGE MLIMANI CITY

Amber Lulu alikuwa mmoja kati ya wageni waalikwa ndani ya ukumbi huo kwenye sherehe maalumu ya siku ya kuzaliwa kwa mama mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim na mchumba wa msanii huyo, Tanasha Donna.

Paparazi wetu ambaye alikuwa ukumbini humo, alimshuhudia mwanadada huyo mwenye makeke mengi akiingia akiwa ndani ya vazi lililoachia eneo kubwa la mwili wake wazi huku akiwa amelewa. “Leo mbona tutaona maajabu. Wamemualika na huyu, ona alivyovaa na anavyotembea vitu viwili tofauti,” alisikika mmoja wa wageni aliyekuwa pembeni wakati Amber anaingia.

AANZA MBWEMBWE

Muda mfupi baada ya kuingia, alikwenda kuketi siti ya nyuma ambapo muda mwingi alikuwa akipiga kelele kwa kushangilia kana kwamba sherehe ilikuwa ikimgusa sana.

Khadija Kopa amvuta Wakati akiendelea na mbwembwe zake nyuma, ulifika muda wa Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa kwenda mbele ya jukwaa na kuimba ndipo uzalendo ukamshinda Amber na kwenda kucheza peke yake. Kelele zilizokuwa zikisikika kila kona ndiyo zilizidi kumchochea zaidi na kujikuta akibinuka staili mbaya ambazo mtu mwenye akili timamu hawezi kuyageuza macho yake mara mbili kumuangalia.

AIBU 100%

Mzuka wa Amber haukuishia hapo, alitoka na kwenda hadi kwenye meza aliyokuwa ameketi mzee Abdul Juma ‘Baba D’ na mkewe na kuanza kuwachezea jambo lililomfanya baba D kufunga macho yake kwa aibu hiyo. “Anamkosea baba D tena mbele ya watoto wake na mkewe ambao wote wapo katika ukumbi huu,” alisikika mmoja wa wageni.

ATAKA KURUDI JUKWAANI

Baada ya kumaliza kucheza mbele ya bab D, Amber alitaka kurudi jukwaani kuendelea kucheza jambo ambalo halikukubaliwa na wageni waliokuwa wakimfuatilia tangu alipoingia. Mwisho wa siku walimrudisha alipokuwa ameketi mwanzoni na kuendelea na kinywaji chake.

AGOMA KUFUNGUKA

Paparazi wetu baada ya kumuona Amber ametulia alimsogelea kujua kulikoni ameamua kujitoa ufahamu mbele ya kadamnasi ambapo alinyanyua glasi yake ya kinywaji kisha akamtazama kwa jicho la hasira.

“Nikuelezee nini sasa hapo? Ulichoona ndicho hicho!” Licha ya kujibu majibu hayo ya mkato, alipobanwa zaidi alipotezea kwa kugeukia upande wa pili na kuendelea kuongea na marafiki zake wengine.

TUJIKUMBUSHE

Amber Lulu ametokea kujizolea umaarufu baada ya kuonekana kwenye video za Kibongo zikiwemo Inde ya Dully akiwa na Harmonize, Bongo Bahati Mbaya ya Young Dee, Too Much ya Darassa na nyingine nyingi. Amber pia anatamba na vibao vingi alivyovitoa kama Watakoma, Jini Kisirani, Only You, Makeke na Vunga.


Loading...

Toa comment