The House of Favourite Newspapers

AMPA KIPIGO MKEWE, AJIUA

MWANAUME mmoja aliyefahamika kwa jina la Patrick, mkazi wa Pongwe mkoani Tanga, amedaiwa kumpiga mkewe na kisha kujiua usiku wa Septemba 16, mwaka huu katika nyumba aliyokuwa akiishi na mkewe maeneo ya Kisima Bora mjini hapo.

 

Ilidaiwa kuwa, Patrick alifikia uamuzi huo kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukwepa usumbufu wa mikono ya sheria baada ya kumpiga mkewe na kuangukia kichwa hadi kupoteza fahamu hivyo yeye kudhani ameua.

 

“Siku hiyo alimpiga sana mkewe, akaangukia kichwa na kuzimia sasa jamaa akadhani ameua ndipo alipoona na yeye ajimalize kwa kujinyonga kukwepa mkono wa sheria,” kilidai chanzo. Risasi Jumamosi lilimtafuta mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Loveness, ambaye alisema siku ya tukio marehemu mume wake alirudi nyumbani kutoka katika shughuli zake akiwa hayupo sawa kama alivyomzoea.

 

Alisema alipomuona yupo katika hali hiyo, alimuuliza kulikoni ndipo marehemu alipoanza kumpiga hadi akapoteza fahamu. “Aliporudi nyumbani mume wangu alikuwa amekasirika ndipo nilipomuuliza nani amekuudhi? Hakunipa jibu, nikawa naendelea kumuuliza zaidi ndipo aliponipiga mpaka nikapoteza fahamu,” alisema Loveness na kuongeza:

 

“Mimi na marehemu mume wangu suala la kunipigana ni jambo la kawaida, nimeshazoea kupigwa na yeye lakini kwa siku ya juzi (Septemba 16) alinipiga kipingo ambacho sikuweza kujitambua kabisa na hadi niliporudisha fahamu ndio nikapatiwa taarifa ya kuhusu mume wangu kuwa amefariki kwa kujinyonga kwa kutumia kamba chumbani.”

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alipotafutwa na Risasi Jumamosi kuhusu tukio hilo alisema yupo likizo na kuomba atafutwe Afande Leonce Rwegasira ambaye anakaimu. Hata hivyo, alipotafutwa Afande Rwegasira, simu yake haikupatikana hewani. Marehemu Patrick aliyeacha mtoto mmoja aliyezaa na Loveness, alizikwa Septemba 17, mwaka huu pembeni mwa nyumba ya mama yake iliyopo maeneo ya Ambangulu, Pongwe

Stori: Zaina Malogo, Risasi Jumamosi

Comments are closed.