The House of Favourite Newspapers

Anguko la Trump Kicheko Afrika

0

UCHAGUZI Mkuu wa Marekani ndio habari ya mjini. Katika matokeo ya awali ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 3, mwaka huu yameanza kuibua kicheko kwa nchi za Bara la Afrika baada na mgombea wa Chama cha Republican anayeyetea kiti chake, Rais Donald Trump kuelekea kuanguka, RISASI JUMAMOSI linachambua.

 

Katika uchaguzi huo, Trump amechuana na mgombea urais kupitia Chama cha Democratic, Joe Biden ambaye ameongoza katika kinyang’anyiro hicho.

Kutokana na hali hiyo, Rais Trump amedai kumetokea udanganyifu katika kuhesabiwa kura na amekwenda mahakamani kutaka mchakato huo usimamishwe.

 

Ili kushinda urais, mgombea anahitaji kupata kura 270 au zaidi zinazotokana na mfumo wa uchaguzi kupitia wajumbe wa majimbo.

Hadi kufikia Novemba 5 jioni, Trump alikuwa amepata kura 214 na Biden alikuwa ameshikilia kura 264. Inakadiriwa kuwa jumla ya watu milioni 160 walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na watu milioni 101.1 waliopiga kura mapema.

 

KICHEKO AFRIKA

Tangu aingie madarakani Novemba 2016, Donald Trump alionekana kuwa kiongozi asiyefungamana na siasa za Afrika kutokana na matamshi yake pamoja na matendo yaliyowapa wakati mgumu Wafrika.

Wachambuzi wa mambo ya siasa za kimataifa wanakumbusha namna Trump alivyowashutumu wahamiaji wanaoingia Marekani kwa kuwatusi.

“Kwa nini tunawaruhusu watu hawa kutoka mataifa ‘machafu’.” Rais Trump aliwaambia wabunge kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post Juni, 2018.

 

Tamko hilo lilidaiwa kuwalenga watu kutoka Afrika, Haiti na El Salvador.

Aidha, katika muendelezo wa kauli zake, Trump aliziita nchi za Afrika kuwa ni nchi chafu ‘nchi za shimo la choo’ kwa kushindwa kujitawala zenyewe.

Hata hivyo, Trump katika uongozi wake alitangaza vikwazo vya utoaji viza kwa raia wa nchi sita ikiwemo Tanzania, kwa kuongeza kwenye orodha ya mataifa ambayo tayari yalilengwa katika mpango wake utata wa marufuku ya kusafiri

Pia, Rais Trump alipendekeza punguzo kubwa la fedha ambazo nchi yake ilikuwa inatoa kwa Umoja wa Mataifa na shirika la misaada la USAid.

Kwenye pendekezo la bajeti hiyo iliyokuwa imepewa jina, America First: A Budget Blueprint to Make America Great Again, Trump aliongeza matumizi ya jeshi hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 54 kwa kupunguza kiwango katika maeneo mengine.

 

WACHAMBUZI KICHEKO…

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Mbwana Allyamtu alisema ni dhahiri anguko hilo la Trump litakuwa furaha kwa Afrika kutokana na siasa zake kuegemea mrengo wa kushoto.

“Ni kweli wakati wa Trump hapakuwepo na uungwaji mkono wa moja kwa moja kwa sababu alijitenga kidogo, alipunguza ule muingiliano wa moja kwa moja kati ya Marekani na Afrika katika masuala ya kiuchumi, kiulinzi na kiusalama.

“Hayo yote ni kwa sababu Trump ni mhafidhina. Yaani mtu mwenye siasa za mrengo wa kushoto, anazingatia masuala ya ndani sana. Ndio maana hakuungwa mkono na nchi nyingi za Asia mbali na Afrika.

“Alijiondoa kwenye mashirika kadhaa ya kimataifa, hata mikataba kama ya kulinda mazingira, kwa hiyo ni mtu ambaye alikuwa akijitenga na dunia ni mtu ambaye alikuwa anaitazama sana nchi yake kuliko Afrika,” alisema.

Alisema anguko lake litakuwa limepunguza kuitenga Afrika. Litaisogeza Afrika na Marekani, kwa sababu wakati wa Obama aliimarisha masuala ya muingiliano wa Marekani na Afrika.

Aidha, aliongeza kuwa licha ya Biden ambaye ana siasa za mrengo wa kulia sawa na Rais mstaafu Barack Obama, hakutakuwa na tofauti kubwa sana.

“Kwa sababu sera za Biden ni kama za Obama ambaye pia kuna baadhi ya mambo kadhaa alitofautana na baadhi ya nchi za Afrika Kaskazini japo aliimarisha muungano na nchi nyingi za Bara Afrika hilo.

 

MFUMO WA UCHAGUZI MAREKANI UPOJE?

Katika mojawapo ya jambo linalowachanganya wengi ni mfumo wa uchaguzi Marekani. Hata hivyo, Mchambuzi wa masuala ya diplomsia, Abbas Mwalimu alilifafanulia RISASI JUMAMOSI kuwa kiuhalisia mchakato huo ulianza zamani.

Alisema ulianza baada ya kongamano la kujadili Katiba ya Taifa hilo mwaka 1788 baadae kuanza kutumika mwaka 1789.

“Ni utaratibu ambao uliwekwa na waasisi wa Marekani. Mmoja wa waasisi aliitwa Hamilton, alishiriki kuandaa maazimio na Katiba ya Marekani.

“Ukiisoma Katiba ya Marekani ibara ya 2(1) inaeleza kuwa uchaguzi utakuwa unafanyika kila juma la kwanza la mwezi Novemba, kwa maana ya Jumanne na kumalizika kila juma ya pili yaani Jumanne ya wiki,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa katiba yao, kuna kura za aina mbili. Kura za wengi ‘majority vote au popular vote’ na kura za wachaguzi au ‘electro vote’.

“Katika kura za wachaguzi, ni kwamba kila jimbo limepewa hadhi ya idadi ya wajumbe wanaopiga kura kumuidhinisha Rais.

“Kura za idadi ya wajumbe hao zinatofautiana kulingana na jimbo husika kati ya majimbo 50 yaliyopo nchini humo. Kila jimbo lina idadi yake licha ya kwamba jumla ya kura au wajumbe ni 538.

Mwanzoni ilikuwa 535 lakini ikaongezwa majimbo matatu ya jimbo la Washington baada ya marekebisho ya pili katika nyongeza ya 17 ya katiba iliyofanyika mwaka 1962,” alisema.

 

WAJUMBE WANAPATIKANAJE?

Akifafanua zaidi alisema mpiga kura anapoingia kwenye chumba cha kupigia kura, anapiga kura ya kwanza ya kumpendekeza Rais ambayo ni maarufu kama ‘popular vote’ kati ya Biden au Trump. Baada ya kura hiyo anapiga kura ya pili ambao ni wajumbe wa baraza.

“Wajumbe wa baraza ambao wapo 538, wanatokana na chama, lakini pili ndio wanaomuidhinisha Rais kwenye mkutano mkuu wa baraza wa mwisho.

“Kila jimbo huchagua wachaguzi au wajumbe wanaowaamini, kutokana na idadi kila chama kinachagua wajumbe 538,” alisema.

Alisema mfumo huo ulitumika ili kuwezesha wachache hao 538 kumuidhinisha Rais kwa kuwa kama angechaguliwa na wamarekani wote angeweza kupatikana rais asiyefaa.

Alisema bada ya kura hizo mbili kufanyika ndani ya juma la kwanza, juma la pili kinachofuata kwa mujibu wa katiba ni wajumbe hao kwenda kukaa kwenye baraza maalumu la wajumbe wanaomchagua rais ‘electro college’.

 

MAJIMBO YANAVYOAMUA MSHINDI

Mwalimu alisema ili kuwa mshindi katika uchaguzi wa urais wa Marekani mgombea hahitaji kushinda kwa wingi wa kura. Badala yake mgombea anahitaji kushinda wingi wa wajumbe katika mfumo unaojulikana kama ‘’electoral college’’ jopo la wajumbe maalum walioteuliwa kulingana na kiwango cha wapiga kura katika jimbo husika na idadi ya watu.

“Mgombea akipata ushindi katika jimbo husika, anashinda kura ya wajumbe waliotengewa jimbo hilo.

Hata hivyo, alisema wajumbe hao wanaweza kufanya mabadiliko Rais ambaye amechaguliwa kwa kura nyingi wanaweza kufanya mabadiliko japokuwa haijawahi kutokea katika historia ya Marekani lakini Katiba imeweka wazi.

“Wale wajumbe wanaweza kubadilisha maamuzi, wale wasiokuwa waaminifu, kwa mfano wanaweza kumpa Trump ambaye ghafla akamshinda Biden.

“Ikitokea itabidi ipelekwe kwenye bunge la Congress, hili liliwahi kutokea kwa rais wa saba wa Marekani, Andrea Jackson ambapo alipigiwa kura zikagongana 270 ndio wakaelekea kwenye bunge hilo.”

STORI: GABRIEL MUSHI

Leave A Reply