Arteta Afichua Jambo Arsenal “Tunatakiwa Kushambulia kwa Haraka”
MIKEL Arteta, amesema timu yake ya Arsenal imekuwa ikiruhusu mabao mengi hasa ikicheza nyumbani kutokana na wachezaji wake kuwa na shauku kubwa ya kupata ushindi, hivyo wapinzani wanatumia nafasi hiyo kufunga.
Arsenal kabla ya mchezo wa jana, ilikuwa imecheza mechi sita za Premier msimu huu, ikiwa haijapoteza, ikishinda nne na sare mbili, huku mechi za ugenini zote ikiondoka na clean sheet, wakati nyumbani ikiruhusu mabao sita.
Arteta alisema: “Tunatakiwa kushambulia kwa haraka, jambo hilo haliwi kwa mtu mmoja pekee, ni timu nzima.
“Tunapokuwa nyumbani, tumekuwa na makosa mengi binafsi ambayo yanasababisha mabao, kitu ambacho ugenini hakijatokea.
“Ukweli ni kwamba, tunapokuwa ugenini tunakuwa na mbinu tofauti kulinganisha na nyumbani.”
Takwimu zinaonesha kwamba, Arsenal imeruhusu bao moja katika mashuti matatu yaliyolenga lango lao wakiwa nyumbani, huku kwa mwaka huu 2023 pekee, ikiruhusu mabao matatu dakika ya kwanza ya mchezo ndani ya Premier League.