The House of Favourite Newspapers

Asante TFF Kwa Buswita, Mechi Chamazi Sawa, TFF Wawe Makini

0
Mchezaji wa Yanga, Pius Buswita.

KWANZA nianze kwa kuwapongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba na Yanga kwa kumaliza suala la mchezaji Pius Buswita na kumruhusu kujiunga na Yanga.

Hiki ndicho nilichosema wiki iliyopita kuwa shida siyo mchezaji mwenyewe, lakini kuna matatizo mengi sana hapo katikati, nashukuru kuona ombi langu kuwa mchezaji huyo anatakiwa kucheza, limetimia.

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Ingawa niwaambie TFF kuwa wanatakiwa sasa kuweka adhabu kali siyo kwa mchezaji tu bali hata yule ambaye amemdanganya mchezaji mwenyewe hadi akasaini mkataba mara mbili.

Siamini na wala siwezi kukubali kuwa Buswita hakushikwa mkono, na kama ni jambo la adhabu basi na huyo mtu wa kati naye aunganishwe, nilisema najua kuwa Buswita ni kijana mdogo na anataka kufanikiwa, hivyo kila kimoja alichokuwa akikifanya alikuwa akikifanya kwa presha kubwa.

Hivyo ni vyema TFF wakaweka msisitizo kwenye hili kwanza lisijirudie tena na pili, kuwe na adhabu kali sana kwa mwingine anayeweza kufanya hivi.

Langu la leo ni suala la TFF kupeleka mechi kati ya Simba na Azam kwenye Uwanja wa Chamazi, kwanza anayeweza kukataa mchezo huu kuchezwa Chamazi atakuwa na tatizo binafsi kwa kuwa Uwanja wa Azam unakidhi vigezo vya kutumika.

Azam wametumia fedha zao nyingi kujenga uwanja kwa ajili ya timu yao, wametumia gharama kubwa ingawa hii ni timu changa, lakini kuna timu kongwe zikiwemo hizo Simba na Yanga ambazo kuanzia mwaka 1935 na nyingine 1936, zimekuwa zipozipo tu na mara kwa mara zilikuja na mipango kuhusu viwanja vyao lakini ikaishia njiani.

Hivyo kwa miaka yote ambayo Azam walikuwa wanakuja Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuwafuata Simba na Yanga lilikuwa ni kosa kwa kuwa kiwanja chao kina vigezo vyote, lakini kuna mambo mengi ambayo TFF wanatakiwa kuyaangalia kwenye mchezo huu, kubwa likiwa suala la usalama.

Uwanja wa Chamazi una uwezo wa kuchukua mashabiki 7000 kwa mujibu wao wenyewe idadi hii ni ndogo sana kwa mashabiki ambao wamekuwa wakiingia kwenye mchezo kati ya Azam na Simba tena kipindi hiki ambacho mashabiki kwa wiki mbili hawakuona mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara, hivyo wana mzuka sana wa kwenda uwanjani.

Kwa hali ilivyo, kwa sasa kama kutakuwa na mashabiki wachache sana ambao watataka kuangalia mchezo huo moja kwa moja uwanjani basi watakuwa 25,000, je hawa TFF watawaweka vipi sehemu ya watu 7000? Hili ni suala la msingi sana ambalo wanatakiwa kulitazama.

Kama watauza tiketi 7000, na kuwaambia mashabiki kuwa tiketi zimekwisha basi watakuwa wamewanyima zaidi ya mashabiki 17,000, haki yao ya kuzitazama timu zao zikicheza jambo pia ambalo siyo zuri sana kwa maendeleo ya soka kwa kuwa dunia nzima mashabiki wamekuwa wakibembelezwa kuingia uwanjani.

TFF wanatakiwa kujua kuwa soka Tanzania haliwezi kuchezwa bila mashabiki, lakini pia kuwazuia mashabiki 17,000 ambao wapo nje nalo ni tatizo kubwa sana kwani itakuwa vigumu na walinzi watatakiwa kufanya kazi kubwa sana na ya ziada.

Kutokana na hivyo, basi TFF wanatakiwa kutumia mchezo huu kama funzo, lakini ni vizuri wakahakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha, pia halikuwa jambo zuri kwa mechi hii kuwekwa usiku, kama kuna uwezekano ingechezwa saa kumi muda ambao mambo mengi yanaweza kuangaliwa na kufanyiwa kazi.

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Leave A Reply