The House of Favourite Newspapers

Askari Polisi Wawili Wafukuzwa Kazi Mwanza

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jonathan Shana, amewafuta kazi askari polisi wawili jijini humo baada ya kubainikka kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa kushirikiana na majangiri.

 

Kamanda Shana amebainisha kuwa askari hao wamekutwa na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya uuzaji wa nyara za serikali aina ya meno ya tembo jambo ambalo ni kinyume na maadili ya jeshi.

 

Amewataja askari hao kuwa ni H. 5461 PC Enock wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoa wa Mwanza na H. 4165 PC Robert wa kikosi maalum, ambao walikutwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 20 katika eneo la Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela mkoani humo.

 

Aidha, Kamanda Shana amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, linaendelea na operesheni maalum kuwasaka waliokuwa wakishirikiana na askari katika biashara hiyo.

 

Askari polisi waliofukuzwa kazi wanashikiliwa na watafikishwa mahakani siku ya ijumaa Agosti 31, 2018 kwaajili ya kufunguliwa mashtaka.

Comments are closed.