The House of Favourite Newspapers

ATCL Yapeleka Marubani Kusimamia Ndege Mpya za Airbus A220 za Kampuni ya Ibom

0
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), imeingia makubaliano ya kupeleka marubani wake kufundisha na kusimamia  ndege mpya za Airbus A220 za Kampuni ya Ndege ya Ibom iliyopo nchini Nigeria.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mha. Ladislaus Matindi, amethibitisha kuwepo kwa makubaliano hayo ambapo amesema ATCL imetoa marubani wake waandamizi wawili ambao watakuwa na jukumu la kuwafundisha  kwa vitendo marubani na walimu wa marubani wa Ibom Air kwa muda wa miezi sita.
“Marubani wa ATCL watakuwa na jukumu la kufundisha na kusimamia mafunzo kwa vitendo hadi watakapojiridhisha kuwa marubani wanafunzi na walimu wao wamefikia viwango vinavyotakiwa kurusha ndege hizo”, alisema Mha. Matindi.
Aidha, Kampuni ya Ibom Air itailipa ATCL gharama za mafunzo hayo kwa mujibu wa mkataba kwa kipindi chote cha makubaliano.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya  ATCL kuonesha uzoefu wa muda mrefu wa kumiliki ndege za Airbus A220-300  na pia kuridhishwa na kiwango cha umahiri wa marubani wa Air Tanzania.
Mafunzo hayo  yanalenga kujenga uwezo kwa marubani wa Ibom Air watakaorusha ndege za Airbus A220, ambazo ATCL ina uzoefu wa  miaka mingi wa kumiliki ukilinganisha na Ibom Air ambao ndio wanaanza kutumia ndege za aina hiyo.
ATCL ina zaidi ya marubani 100 na inamiliki ndege aina ya Boeing B787-8, B737 MAX 9, B767-300F, Airbus A220-300 pamoja na Dehaviland  Q400 na Q300.
Leave A Reply