ATHARI KIAFYA ZA KUTOKUNYWA MAJI YA KUTOSHA!

WATU wengi wanadharau maji ya kunywa, wanaona kula ndio muhimu kuliko kunywa maji. Wanaona vinywaji vingine ndio bora kuliko kunywa maji. Hawajui ni hasara kubwa kiasi gani wanajisababishia katika miili yao kwa kutokunywa maji ya kutosha. Ni wengi ambao hawathamini maji ya kunywa kabisa, wengine huweza kushinda siku nzima bila kunywa maji jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.  Leo tutawaletea athari kubwa za kutokunywa maji au kunywa kidogo. Kutokunywa maji hufanya ngozi kuwa kavu na kuleta makunyanzi mwili mzima na huua nuru ya macho na kusababisha matongotongo mengi machoni na kufanya wekundu na utando machoni na kusababisha kutokuona vizuri na kulazimika ufikiche jicho ndio uone.

Pia kutokunywa maji husababisha chunusi usoni na mwilini, mgongoni, mapajani, mabegani, makalioni na hata shingoni. Kama huna maji mwilini uchafu au sumu inabakia katika figo na husababisha kuua figo ambazo zinahitaji maji ili kutoa uchafu unaojikusanya ndani yake. Uchafu unaobakia huleta madhara makubwa kiafya. Kutokunywa maji husababisha mdomo kutoa harufu mbaya na ngozi ya kichwa huwa kavu na kufanya mzizi wa nywele kukosa nguvu na nywele kutoka nzima nzima na pia kukatikakatika.

Ukosefu wa maji mwilini husababisha kupunguza damu na kuharibu mzunguko mzima wa hedhi kwa mwanamke na pia hata unapopata siku zako uchafu hautoki vizuri. Kukosa maji mwilini husababisha mkojo kuwa wa njano pia kuwa na harufu kali sana na husababisha magonjwa mengi ya ngozi, kupatwa kwa mzio (allergy) bila ya kutegemea.

Kutokunywa maji ya kutosha husababisha kutokupata haja kubwa au kupata ngumu na husababisha mchubuko katika njia ya haja kubwa na mgonjwa kupata ugonjwa wa bawasiri. Usipokunywa maji husababisha kukosa usingizi na kuleta weusi machoni na pia kuumwa kichwa mara kwa mara na kuwa na harufu mbaya ya jasho.

Ukosefu wa maji mwilini husababisha mwili kuchoka na kujisikia kukosa nguvu na pia kukosa hamu ya kula, kushusha presha na sukari mwilini. Mwili huuma kama mtu aliyepigwa na fimbo. Pia husababisha dawa yoyote ya kupaka katika ngozi iwe cream au lotion au dawa ya tiba yoyote kutokufanya kazi kwa sababu tayari wakati huo ngozi inakua dhaifu na kukosa virutubisho.

Usipokunywa maji ya kutosha unasababisha kupata U.T.I na matatizo mengi katika kibofu na mwishowe kuathiri kizazi, pia husababisha kuumwa sana kwa miguu na nyayo, hasa sehemu za kisigino na pia mishipa kuvutana na kuuma sana wakati wa kulala au kukaa. Kwa kweli madhara ya kutokunywa maji ni mengi, haya ni baadhi tu. Bila shaka unakubali sasa kwamba maji ni kitu muhimu sana katika mwili wa binadamu.

USHAURI

Unatakiwa unywe maji kulingana na uzito wako; mfano lita mbili kama una kilo 50, lita tatu kama una uzito wa kilo 65, lita nne kama una kilo 80 n,k kwa siku na ni lazima kunywa maji kila siku. Kukaa bila kunywa maji ni hatari sana kwa afya yako.

Anza kwa kunywa maji kiasi na polepole hadi kufikia lengo lako kwa kuzingatia uzito wako. Unaweza kuweka matunda freshi ndani ya maji ili kupata ladha na kukupa hamu ya kunywa.


Loading...

Toa comment