The House of Favourite Newspapers

Azam FC dhidi ya Yanga SC Kitawaka Leo Sikukuu ya Krismasi Uwanja wa Mkapa

0

HERI ya Sikukuu ya Krismasi kwako msomami wa Spoti Xtra, leo Jumapili, wakati unasherehea sikukuu hiyo, utapata burudani tosha kutoka kwa wakali wawili kunako Ligi Kuu Bara, Azam FC dhidi ya Yanga SC.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Azam watakuwa wenyeji baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa uwanjani hapo kumalizika kwa sare ya 2-2.

Cedric Kaze, Kocha Msaidizi wa Yanga, amesema mchezo wao dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu, lakini wamefanyia kazi makosa waliyofanya kwenye mzunguko wa kwanza hasa katika mipira ya adhabu.

Kaze amebainisha kuwa: “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC, kila mmoja atafanya kazi yake ili kupata matokeo na tunakumbuka mchezo uliopita tulipata pointi moja huku Azam FC mabao yao wakifunga kutokana na matumizi ya set pieces (mipira iliyokufa).

Kikosi cha Azam.

“Kwa makosa ambayo tulifanya kwenye mchezo uliopita na mechi zetu ambazo tumecheza tumefanyia kazi na tunaamini kwamba tutapata matokeo mazuri, tunahitaji kuongeza pointi ili kuzidi kuwa karibu na kutwaa ubingwa.”

Kwa upande wa beki wa Yanga, Dickson Job, alisema: “Zawadi tutakayotoa kwa mashabiki ni ushindi na tumekuwa tukipata matokeo kwenye mechi zetu kutokana na ushirikiano pamoja na mbinu ambazo tunapewa na benchi la ufundi.”

John Matambala, Kocha Msaidizi wa Azam FC, alisema wanatambua mchezo utakuwa mgumu na kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

Kikosi cha Yanga.

“Tunatambua kwamba ushindani utakuwa mkubwa, lakini ukweli ni kwamba tunawaheshimu wapinzani wetu na tunaamini utakuwa mchezo mzuri,” alisema.

Lusajo Mwaikenda, nyota wa Azam FC, alisema kuwa wana wachezaji wazuri na imara kwenye safu ya ushambuliaji jambo litakalowapa matokeo.

“Ushindani ni mkubwa na kila mmoja anatambua uhitaji wa pointi tatu muhimu kwenye mchezo wetu, wachezaji tupo tayari na tunawashambulaji wazuri,” alisema.

Leave A Reply