The House of Favourite Newspapers

Baadhi ya Makosa Aliyoyafanya Mwl. Nyerere

 julius_nyerere

Na Walusanga Ndaki

TATIZO la Watanzania wengi  — wazee kwa vijana — ni kwamba ukianza kuwaorodheshea makosa aliyoyafanya aliyekuwa kiongozi wa nchi hii, Julius Nyerere, watakununia na kukuona humtendei  haki binadamu huyo ambaye alifariki miaka 17 iliyopita Oktoba 14, 1999.

Nyerere hakuwa mtu wa kawaida katika jamii yetu; alikuwa ni  kiongozi wa nchi hii yenye mamilioni ya watu aliyoitawala kwa miaka ipatayo 25, hivyo kujadili mema na mabaya aliyoyafanya, ni kawaida na kwa faida mbili. 

Kwanza,  ni kwetu kuendeleza mema aliyoyafanya, hata kama hatutakuwa viongozi.  Pili,  ni kuweka tahadhari makosa aliyoyafanya asiyerudie  mtu mwingine, hususan viongozi!

Pia, ni kuwatendea haki watoto na wajukuu zetu ambao hawakumfahamu Nyerere kwa kuwaeleza sura zote mbili za mtu huyo, kwani naye alikuwa binadamu na alikiri kwamba alifanya mema na mabaya, akawasihi  Watanzania wafuate yaliyowafurahisha, waachane na yaliyowatia simanzi.

 Nyerere hakuwa na uchu au tamaa ya utajiri, jambo wanalolifahamu hata maadui zake.  Lakini, kisiasa – kama wanasiasa wote duniani — Nyerere alikuwa anapenda madaraka, la sivyo asingetawala kwa miaka 25 akiwaamulia wananchi wenzake mambo kibao, yaliyowafurahisha na yaliyowakasirisha.

1104-1-1-julius-nyerere

Kosa kubwa la kwanza alilofanya Nyerere ni kujikita mno katika siasa na kuyapa kisogo mambo muhimu kwa jamii.  Alidhamiria mno ‘kuwalewesha’ Watanzania kisiasa hadi akaanzisha somo la Elimu ya Siasa (Political Education) mashuleni, majeshini na  taasisi mbalimbali ili kudhoofisha elimu kwa malengo ya kisiasa.

Kosa kubwa la pili ni kuanzisha siasa ya Ujamaa chini ya Azimo la Arusha mwaka 1967, ambapo uzalishaji mali – tangu bucha za kuuza nyama mitaani, kumbi za starehe, viwanda vya Chibuku hadi vya kuunganisha magari – vikawa vinaendeshwa na serikali!

Waliokuwa watu wazima, watakumbuka watu walivyopanga misululu nchi nzima kununua sukari, mkate, sigara, mchele, chibuku na kadhalika.  Ni kwa vile bidhaa zote muhimu vyote zilikuwa vinazalishwa na kuuzwa na serikali, hivyo kusababisha upungufu!

Hili lilizuia watu binafsi kushiriki katika uchumi, matajiri wakawa maadui wa taifa, wakiitwa wanyonyaji, makupe na manyang’au! Wanasiasa wakawa wafalme,  wakipanga na kupangua walichokitaka, wakasahau siasa za kweli ni zinazompa mtu shibe na malazi,  si za paradiso au peponi  zenye majina ya Ujamaa, Ukomunist au Usoshalist ambazo leo hii zinaonekana kichekesho!

Nyerere hakugundua kwamba siasa ni michezo inayobadilika, haipaliliwi na kubaki  mioyoni na akilini.  Siasa za kufikirika zilizokuwepo Urusi ya Kisoviet, China, Ujerumani Mashariki na kwengine, leo zimetokomea na zilikobakia, watu wake wanaishi katika majonzi yasiyo ya mkombozi!

Siasa hizohizo zilimfanya aufute mfumo wa vyama vingi mwaka 1965, mfumo ulioanza wakati wa uhuru mwaka 1961.  Ni ajabu aliufuta ukiwa tayari umeanza kukomaa na kuota mizizi!

Alitunga katiba mbalimbali ikiwemo ya  sasa ya  mwaka 1977 ambayo hata mwenyewe alisema ni ya kidikteta na kwamba mtu angeitumia kuwa dikteta wake. 

Ni katiba hiyohiyo iliyomfanya akawa anagombea urais peke yake bila mpinzani angalau hata kutoka chama chake ambapo wananchi waliwajibika tu kumpitisha au kumkataa kwa kukubali maneno NDIYO au HAPANA!

Ni ajabu kwa nini aliitunga na kuitumia na kwa nini, kama kweli ilikuwa ni ya kidikteta, hakuifuta wakati anaondoka madarakani?

Katiba hiyo inaendelea chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa  chimbuko la migogoro mingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii sasa chini ya vyama vingi vya siasa.

Katiba hiyo iliyompa Nyerere madaraka kibao, inaendelea leo kumpa rais madaraka kama hayo ya kuteua watu awatakao katika nafasi zote nyeti na muhimu nchini, tangu wakuu wa idara, wilaya, mikoa, mawaziri, wakuu wa vyombo vya usalama na ulinzi.  

Hii ni pamoja na kuteua Tume ya Uchaguzi aitakayo, ambapo kauli yake ya  mwisho kwa uchaguzi wa urais haipingwi popote na yeyote!

Mitafaruku kuhusu Muungano ni mabaki hasi ya makosa ya Nyerere ambapo hakutaka yajadiliwe na kupewa ufumbuzi, hususan baada ya kubaki peke yake kufuatia kifo cha Abeid Aman Karume.

Matatizo ya kiuchumi yaliongezwa na vita dhidi ya Idd Amin wa Uganda iliyopanga kumrejesha madarakani aliyekuwa rais wa Uganda na rafiki wa Nyerere, Milton Obote, aliyekuwa amekimbilia Tanzania.  Obote alirejea madarakani, lakini Waganda walimpindua tena akakimbilia Zambia alikofia baadaye.

Akitetea Ujamaa, Nyerere alikataa masharti ya Shirika la Fedha Duniani (IFM) ambayo yangeiokoa nchi kiuchumi, masharti yaliyokuja kukubaliwana rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi. Kuchelewa huko kumeifanya leo Dola moja ya Marekani kukaribia Sh. 3,000 tofauti na majirani zetu kama Kenya ambao uchumi wao haukufuata itikadi za kufikirika.

Mwinyi aliyaelewa zaidi mazingira ya kweli duniani, akaachana  na Azimio la Arusha ambalo wanafiki wachache (hususan wanasiasa)  ‘wanalijutia’ leo wakifikiri lingewajengea heshima kama ya Nyerere!

Wapenzi na wakosoaji wa Nyerere, watakumbuka alipenda kunukuu msemo wa Kiingereza wa: “Power corrupts, absolute power corrupts absolutely.”  Hii ikimaanisha kwamba: “Madaraka hulewesha, na madaraka makubwa zaidi hulewesha zaidi.”  Hakika, madaraka hulewesha!

Ni Julius Kambarage Nyerere ambaye Watanzania wengi – hususan wasomi, wema na waovu  – wanalitumia  jina lake kwa sifa lakini kamwe hawaishi kama alivyoishi kwa kujishusha.

Comments are closed.