The House of Favourite Newspapers

Baba Kanumba Alalamikia Hukumu ‘Ndogo’ Dhidi ya Lulu

0
Mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’.

BAADA ya Mahakama Kuu kumhukumu mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwenda jela miaka miwili kwa kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwigizaji Steven Kanumba, baba wa Kanumba, Charles Kanumba, amelalamikia hukumu hiyo akisema ni ndogo mno.

 

Baba wa Kanumba, Charles Kanumba.

Mwandishi wa Global TV Online, Isri Mohammed, leo amefanya mahojiano kwa njia ya simu na mzee Kanumba akiwa nyumbani kwake mkoani Shinyanga, kama yalivyo chini:

 

Isri:  Hallow!

Baba Kanumba; Nani mwenzangu?

 

Isri:  Shikamoo baba, naitwa Isri kutoka Global TV Online.

 

Baba Kanumba: Ipo wapi hiyo Global TV?

 

Isri:  Global TV Online ipo jijini Dar es Salaam.

 

Baba Kanumba: Ipo Dar! Mlikuwa na shida gani?

 

Isri: Tulitaka kujua maoni yako baada ya Mahakama kutoa hukumu kwa  Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa miaka miwili kwa kumuua bila kukusudia aliyekuwa mtoto wako Steven Kanumba.

 

Baba Kanumba:  Kwa upande wangu hukumu hii kwa nini imekuwa ndogo sana?  Na haijanifurahisha sana hata kama mtu aliua kwa kutokukusudia lakini mahakama imetoa kifungo cha miaka miwili, kama mtu kaua kuku.

 

Isri:  Baba kwa upande wako ulitaka mahakama itoe kifungo cha muda gani kukufurahisha?

 

Baba Kanumba: Nilitegemea mahakama ingetoa kifungo kuanzia miaka mitano, sita au saba na kuendelea.

 

Isri:  Kwa nini baba hujatokea kwenye hii kesi kuungana na mke wako mahakamani?

 

Baba Kanumba: Sikuja huko, nilimwachia mke wangu aendelee na kesi hiyo kutokana na kupunguza gharama zisizo za msingi na ndo hivyo hukumu yenyewe ni miaka miwili tu kama kaua kuku.  Si ningepoteza muda wangu tu hapo na hukumu yenyewe isingenifurahisha kulingana na mazingira ya kifo cha mtoto wangu.  Je, namba yangu mmeitoa wapi?

 

Isri: Sisi tunafanya kazi ya uandishi na hivyo kufuatilia kila kitu kinachotokea ikiwa ni pamoja na kujua namba za watu wanaohusika na kazi zetu.  Hivyo usiwe na wasiwasi kwamba namba yako tulikuwa nayo.

 

Baba Kanumba: Nawashukuru, hata hivyo, mimi sina hofu na nawashukuru kwa kunipigia.

(HABARI NA ISRI NA NICOLAUS TRAC/GPL)

Leave A Reply