The House of Favourite Newspapers

Baba miaka 55 alia: BINTI WA MIAKA 17 KANIPONZA

SIWEZI kusahau tukio hilo katika maisha yangu yote, binti wa miaka 17 kaniponza na kuniharibia maisha yangu yote.  “Mguu wangu umekatwa, nimekuwa mtu wa kutembelea magongo,” ndivyo Jumanne Hassan (55) Mkazi wa Kihonda Dodoma, alivyoanza kumsimulia mwandishi wetu mkasa mzito uliompata katika maisha yake.

ILIKUWAJE?

Jumanne anaeleza kuwa mwaka 1995 akiwa kijijini kwao Kihonda alimpenda binti mmoja aliyekuwa akiitwa Hawa ambapo mbali ya kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi aliamua kwenda kwao kujitambulisha kwa lengo la kumuoa. “Nikaambiwa nitoe mahari, nikatoa. Baadaye tukafunga ndoa na tukaanza kuishi tukiwa ni mume na mke,” alisema Jumanne.

KILICHOTOKEA BAADA YA KUOANA

Jumanne anaeleza kuwa, siku chache baada ya kuanza maisha yao ya ndoa, mkewe alimwambia kuwa kuna mmoja kati ya viongozi wa kijiji hicho hakupendezwa na ndoa yao. “Nilipomuuliza kwa nini? Aliniambia kuwa kiongozi huyo (jina linahifadhiwa) naye alikuwa akitaka kumuoa Hawa lakini alimkataa.

“Basi tukawa tunaishi hivyo lakini chokochoko kutoka kwa kiongozi huyo zilizidi, kuna siku alinitamkia kuwa atanikomesha kwa sababu mimi siwezi kumzidi ujanja.” Jumanne anaendelea kusimulia kuwa hakujua kukomeshwa huko kungekuja kwa njia gani lakini siku moja alishtukia polisi wanafika nyumbani kwake na kumtia nguvuni kwa maelezo kuwa nimeoa binti aliye chini ya miaka 18 na hivyo yeye ni mbakaji.

“Kusema kweli nilishangaa kwa vile kijijini kwetu wanaume wengi tu walikuwa wameoa mabinti wenye umri kama wa mke wangu na hawakukamatwa. “Nikawaambia polisi huyu ni mke wangu na ninaishi naye kihalali; wakasema mimi ni mbakaji,” alisema Jumanne kwa masikitiko.

JUMANNE KIZIMBANI

Awali Jumanne aliona kama mambo yatakuwa ya mzahamzaha na kwamba suala la litamalizwa kirahisi, lakini jambo ambalo halikutokea. Siku chache baada ya kukamatwa alipandishwa kizimbani mjini Dodoma kujibu tuhuma za ubakaji huku akianza rasmi safari ya kuishi mahabusu kwa vile alikosa dhamana.

 

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA

“Kesi imeendelea mahakamani hadi mwaka 1999 ambapo nilihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. “Nilianza kutumikia kifungo kwenye gereza la Dodoma, baadaye nikapelekwa Singida na kisha kuletwa Dar es Salam.

“Nikiwa Dar nilipelekwa kwenye magereza tofauti ikiwemo Keko, Ukonga na Segerea. Mazingira ya maisha yalikuwa magumu kama unavyojua nikajikuta nimepata fangasi za mguu. “Ikabidi nipelekwe Hospitali ya Muhimbili, nilitibiwa lakini sikufanikiwa kupona, madaktari wakasema mguu umeoza na hivyo ni lazima ukatwe.

“Hiyo ilikuwa ni habari mbaya sana kwangu, nakumbuka nililia sana siku hiyo nikakumbuka maisha niliyokuwa nayo na jinsi nilivyojikuta matatani kwa kosa la ubakaji. “Sikuwa na cha kufanya ukatwe na kuanza maisha ya ulemavu kama hivi unavyoniona.”

APATA TATIZO LA KIBOFU

Wakati akiendelea kuhangaika na mguu, Jumanne anasema alianza kusumbuliwa na tatizo la kibofu cha mkojo ambalo lilizidi kudhoofisha afya yake. “Kwa bahati mwezi wa sita mwaka huu nilitoka gerezani kwa msamaha wa Rais Dk John Pombe Magufuli, nikatoka nikiwa sina mguu, nilipofika uraiani ni kama nilikuwa naanza maisha mapya kutokana na muda mwingi kuishi gerezani.”

ARUDI NYUMBANI AKUTA MAJANGA

Jumanne anasema aliporudi nyumbani kwao alikuta mambo mengi yameharibika baadhi ya ndugu zake walikuwa wameshafariki dunia na kwamba hata aliowakuta hawakuwa katika hali nzuri kimaisha.

“Kulinagana na mazingira niliyoyakuta huko Dodoma, niliona nikiendelea kukaa huko nitakufa mapema, ikabidi nije Dar es Salaam kwa lengo la kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda ili aweze kunisaidia.

“Lakini toka nimefika nahangaika tu sijafanikiwa kumuona, hapa nilipo nimehifadhiwa kwa msamaria ambaye ni dereva pikipiki, sijui cha kufanya,” alisema Jumanne.

Alimuomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Ally Mwalimu kutoa elimu hasa vijijini kuhusu umri wa binti kuolewa vinginevyo wanaume wengi watajikuta wakipata matatizo kama yake.

AOMBA MSAADA

Kutokana na maisha magumu aliyonayo anawaomba Watanzania waweze kumsaidia ili angalau aweze kupata fedha kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa kibofu unaomsumbua na ikiwezekana apate mtaji wa kufanya biashara ndogondogo.

Kwa yeyote ambaye ameguswa na mateso ya Jumanne anaweza kuwasiliana naye kwa namba za simu 0678947789, jina la usajili wa namba hiyo ni Omari Juma.

Comments are closed.